The House of Favourite Newspapers

Hamisa Mobetto Atolewa Mahari Na Aziz Ki Viwanja vya Gofu, Mikocheni

Mtangazaji na muamasishaji wa mambo mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii Burtoin Mwenda ‘Mwijaku’ akiwakarihisha upande wa Azizi Ki walipowasili kabla ya tukio la mahari.

Mwanamitindo, muigizaji na msanii wa muziki wa Kizazi Kipya nchini Tanzania, Hamisa Mobetto leo, Februari 15, 2025 kupokea mahari ya kifahari ya ng’ombe 30 kutoka kwa mchumba wake, nyota wa klabu ya Yanga SC na raia wa Burkina Faso, Stephanie Aziz Ki.

Tukio hilo la kihistoria limefanyika kwenye Viwanja vya Gofu, Mikocheni, jijini Dar es Salam na likihudhuriwa na watu maarufu kibao.

Rais wa Yanga SC, Injinia Hersi Said, aliongoza hafla hiyo kwa niaba ya familia ya Aziz Ki, akiwakilisha mahari hiyo kwa familia ya Hamisa.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wachezaji kadhaa wa Yanga, akiwemo nahodha Bakari Mwamnyeto, Pacome Zouzoua, na Yao Kouassi, pamoja na maafisa wa klabu hiyo akiwemo Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe.

Hamisa, aliwasili eneo la tukio akiwa na meneja wake, Paul Mangoma, huku akisindikizwa na warembo 15 waliovaa sare za kuvutia.

“Siku ya leo ni baraka kubwa maishani mwangu,” alisema Hamisa mbele ya umati. “Namshukuru Mungu kwa kunipa mpenzi ambaye si tu mwaminifu bali pia mwenye mapenzi ya dhati. Tumepanga mambo mengi mazuri, na namuomba Mungu aongoze safari yetu hadi kwenye ndoa na maisha ya furaha.”

Ndoa hiyo imepangwa kufungwa kesho Jumapili, Februari 16, 2025, inatarajiwa kuwa moja ya hafla kubwa zaidi za mwaka, huku sherehe rasmi zikitarajiwa kufanyika Februari 19, kwenye ukumbi wa kifahari wa The Super Dome, Masaki jijini Dar.

Mwanamitindo, muigizaji na msanii wa muziki wa Kizazi Kipya nchini Tanzania, Hamisa Mobetto