×

Pluijm: Nipo tayari kumpokea Niyonzima

pluijm1Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm.

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm, amesema yupo tayari kumpokea kiungo wa timu hiyo Myarwanda Haruna Niyonzima na kufanya naye kazi tena, endapo atamalizana na uongozi.

Niyonzima alisimamishwa na klabu hiyo kutokana na utovu wa nidhamu na baadaye ikatangazwa kuwa mkataba wake umevunjwa, lakini hivi karibuni aliomba msamaha na kuna taarifa kuwa ameshasamehewa na uongozi wa timu hiyo.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Pluijm alisema hana shida na mchezaji huyo na yupo tayari kumpokea na kuendelea kufanya naye kazi endapo tu uongozi utamalizana naye.

“Mimi sina shida na Niyonzima, ni mchezaji wangu na alikuwa anafanya vizuri sana kwa kipindi chote alichokaa hapa klabuni.

“Nipo tayari hata kesho kufanya naye kazi kama atakuwa amemalizana na uongozi masuala yake ya utovu wa nidhamu, nitakachofanya ni kaa naye chini na kuongea naye ili asirudie tena, lakini hakuna kizuizi chochote kwangu,” alisema Pluijm raia wa Uholanzi.

Taarifa zimekuwa zikisema kuwa kiungo huyo ameshamalizana na uongozi wa Yanga na kuna uwezekano mkubwa sana akaanza mazoezi na timu hiyo siku chache zijazo.

Leave a Comment