×

Hakimu Ampa Masharti Mwampamba

DUSTAN SHEKIDELE, AMANI

MOROGORO: Mwisho Mwampamba, mshiriki wa Shindano la Big Brother Africa 2003, ambaye alishtakiwa na kaka yake kwa kumtukana matusi ya nguoni, ameomba radhi kortini mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Chamwino, Amina Chungulu, akitaka afutiwe kesi hiyo ili shauri hilo limalizwe kifamilia.

Kesi hiyo namba 197, ilisikilizwa mara ya pili Jumatatu iliyopita, baada ya Robert Mwampamba kumshtaki ndugu yake huyo anayedaiwa kumtusi kupitia mitandao ya kijamii.

Mwisho alimuomba msamaha kaka yake akidai hatarudia tena kosa hilo na hakimu Amina alipomuuliza kaka mtu kama ameridhia ombi hilo, alikubali lakini akatoa masharti yaliyokubaliwa na mlinzi huyo wa amani, kwamba shauri hilo lisifutwe hadi hapo matusi yaliyopo katika mitandao hiyo ya kijamii yatakapokuwa yameondolewa katika akaunti za mshtakiwa.

Hivyo hakimu huyo aliisogeza mbele kesi hiyo hadi Aprili 28, mwaka huu itakaposikilizwa tena ili kutoa uamuzi wake.
Mwisho aliyejipatia umaarufu mkubwa nchini baada ya kushiriki shindano hilo mara mbili ni mmoja wa watoto wa marehemu Dk. Ephraim Njawala Mwampamba aliyekuwa akijulikana sana mjini Morogoro aliyefariki Februari mwaka huu na kuzikwa kijijini kwao, Uyole Mbeya.

Leave a Comment