Saimeni Mgalula, Amani
SONGWE: Kitengo cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers wiki hii kiliifungia kazi baadhi ya mitaa ya Tunduma wilayani Momba mkoani hapa ili kubaini maeneo ambayo biashara ya ngono (machangu kujiuza) imeshamiri kufuatia maombi ya wakazi wengi wa hapa.
Katika oparesheni hiyo iliyofanyika kwenye mitaa kadhaa ya ndani ya mji wa Tunduma, OFM iligundua baadhi ya maeneo ambayo machangudoa wamekuwa wakipiga kambi za kibiashara huku wateja wakiwafuata huko kwa siri.
Katika Mtaa wa Valentini, OFM ilifika kwa wakati na kuzungumza na baadhi ya vyanzo makini vya habari ambapo chanzo kimoja (jina limehifadhiwa) kilisema kuwa ni kweli maeneo hayo yamekuwa yakitumika kwa biashara hiyo hasa nyakati za usiku mnene ndiyo kunakucha zaidi.
“Unajua mji wa Tunduma upo mpakani mwa nchi jirani ya Zambia na Malawi hivyo kumekuwa na mchanganyiko wa watu tofauti ambapo dada zetu ndo’ wameamua kulifanya eneo hilo kuwa la kujiuza ili kupata fedha za kuendeshea maisha yao,” kilisema chanzo hicho.
Kikaendelea: “’Tena baadhi ya dada zetu na wengine wamama wa makamu wamekuwa wakitoka mbali kama Mbeya, Iringa na kuja kujiuza hapa Tunduma. Kwa upande wa dada zetu wa hapa nyumbani ambao ni wenyeji ni wachache sana.”
Inaelezwa kwamba, kwa mchana hakuna anayeweza kujua kama mji huo ndivyo unavyokuwa usiku kutokana na pilikapilika za maisha ya kila siku na wao machangudoa wanakuwa wamelala.
OFM pia ilitembelea maeneo mengine ya Mtaa wa Afrikana na Kampala ambapo wenyeji wa eneo hilo walikiri kushamiri kwa biashara hiyo ya ukahaba hususan nyakati za usiku.
OFM ilipiga hodi kwenye ofisi za wenyeviti wa mitaa yote ili kusikia viongozi wanasemaje kuhusu kushamiri kwa machangudoa hao ambapo hata hivyo, hakuna aliyepatikana na waliokutwa walisema wao si wesemaji.