KWA mara ya kwanza muziki wa Taarab unatarajiwa kutikisa kesho Jumamosi kwenye Ukumbi wa Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar katika bonge la shoo lijulikanalo kama Usiku wa ya Kale ni Dhahabu.
Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo amesema itakuwa ni historia kwa muziki huo kwani kwa mara ya kwanza Dar Live pekee itawakusanya wakali kibao kama vile Leila Rashid, Mzee Yusuf pamoja na Bi Shakira.
“Haijawahi kutokea lakini kesho kwa mara ya kwanza historia itaandikwa Dar Live kwa wakali kibao wa Taarab kama Hadija Yusuf, Bi Mwanahawa, Joha Kassim kutoka Jahazi Modern, Hadija Kopa, Otham Sudi, Mwanaidi Shaban kutoka Muungano, Shakira kutoka J.K.T, Misambano na Kisauji kutoka Babloom,” alisema Mbizo.
Wakali wengine wanaotarajiwa kuwepo ni Sabaha Mchacho, Sihaba Juma, Hassan Soud, Thabit Abdul, Bi Afua, Sizya Mazongela, Mustafa, Sihaba Juma, Zubeda Mlamali na wengine kibao.
Shoo hiyo imedhaminiwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi Airtel, kupitia huduma yao ya kijanja ya kimawasiliano ya Airtel Money Tap Tap inayopatikana jijini Dar kwa sasa.
