
NA HAMIDA HASSAN | AMANI | HABARI
DAR ES SALAAM: Sherehe ya kitchen party ya msanii wa sinema za Bongo, Coletha Raymond ‘Koleta’ iliyofanyika nyumbani kwa wazazi wake, Makongo mwishoni mwa wiki iliyopita, ilijaa vituko kadhaa hali iliyowafanya baadhi ya waalikwa kuondoka huku wakinung’unika.
Sosi wa habari hii aliliambia Gazeti la Amani kuwa, awali ya yote kituko kilichowafanya waalikwa wajiulize kulikoni ni vazi alilovaa bi harusi huyo mtarajiwa ambalo kwa hakika kutoka mioyoni mwa waalikwa, walisema ni shela (gauni la harusi) na ile ni kitchen party (gauni la kitenge linahusu sana).

Msikie sosi
“Jamani jamani! Sherehe ya Koleta naona imefunga mwaka kama siyo kuufungua, naona mwenzetu yule aliamua kuvaa shela kwenye shereye ya kitchen party! Loo! Mimi naona ile si hali ya kawaida maana imezua minong’ono ile mbaya,” mwalikwa mmoja aliliambia Amani hivyo.
Ahesabu pesa za kutuzwa
Funga kazi ni kituko kingine ambacho kiliwashangaza wengi ni pale bi harusi huyo alipoamua kusitisha shughuli hiyo kwa muda na kuomba ahesabu mwenyewe minoti aliyotuzwa na watu huku akisema kuwa, anahisi kudhulumiwa.
“Watu walijiuliza anadhulumiwa nini wakati pesa yenyewe ni ya zawadi tu na yeye aliomba atuzwe. Je, wasingetoa angekwenda polisi kuwashtaki? Hamuwezi kuamini baada ya kuzihesabu ndiyo roho yake ilitulia na kusema zimekamilika. Kitendo hicho nacho kiliwashangaza wengi kwani mabibi harusi wote huhesabiwa pesa na matroni wao,” alisema sosi wetu.
Shughuli ilipangwa iwe ya milioni 16
Taarifa za awali zilidai kuwa, shughuli hiyo ilipangwa igharimu shilingi milioni 16 huku kila mmoja akiambiwa achangie elfu hamsini lakini cha kushangaza ilifanyika nyumbani kwao na watu walikuwa wachache.
“Hiyo nayo ni sehemu ya kituko kwani inaonekana bi harusi alipania mambo ndiyo maana akaamua kuifanya. Hata hivyo, michango haikutosha na shughuli iliyofanyika haikufikia gharama ya hata shilingi milioni tatu,” alisema mtoa habari huyo.
Wasanii waisengenya shughuli
Baadhi ya wasanii walisikika wakiisengenya sherehe hiyo kwa kusema kuwa, watu hawakumchangia Koleta kwa sababu na yeye huwa hajitoi kwenye shughuli za wenzake.
Amani liliona usawa wa habari hii, upo kwa kumpata Koleta mwenyewe na kumsomea mashitaka yote dhidi yake ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Kuhusu kutotokea shughuli za wenzangu, hakuna msanii yeyote aliyewahi kunialika halafu sijachangia. Waliojitolea kwa udogo wao ndiyo marafiki zangu, mimi sina rafiki.
“Halafu ninavyojua mimi, kitchen party hufanyika nyumbani. Kuhusu shela, watu waangalie vizuri (angalia picha msomaji) hili gauni si shela, ni gauni jeupe.”