
“Ulikuwa unaongea na nani?” aliuliza huku akionekana kuwa na hasira kali.
“Rafiki yangu!”
“Ndiyo ukaongelee chooni!”
“Jamani! Si mambo yetu ya kikekike mpenzi! Kama nimekukera naomba unisamehe bebi…” alisema Fareed, alizungumza kwa sauti nyembamba mno ambayo aliamini ingeufanya moyo wa mwanaume huyo kulainika, hakutaka mwanaume yule aliyekuwa akizungumza naye ajulikane, akajitahidi kuificha simu yake na kisha kuanza kumbusu Godfrey, alianzia mashavuni na kuhamia mdomoni, yote hayo ilikuwa ni kumsahaulisha na kile kilichokuwa kimetokea.
“Umekasirika mpenzi?” aliuliza Fareed.
“Usijali! Ila siku nyingine jitahidi kuwa muwazi,” alisema Godfrey na kisha wote kupumzika kitandani.
“Kesho ndiyo kesho! Ni lazima nikaonane na huyo bilionea, nimchune mpaka achunike,” alisema Fareed huku akiachia tabasamu pana, hakutaka kuwa na Godfrey, kwanza alitaka kuwa na nafasi ya kujaribu asali ya mzinga mwingine.
***
Akili ya Fareed ilichanganyikiwa, kichwa chake kilifikiria pesa na hakutaka kuona akiwaacha wanaume hao na wakati aliambiwa kwamba walikuwa na pesa, mabilionea wakubwa wa mafuta huko Dubai.
Alilala na Godfrey lakini kichwa chake hakikutulia hata mara moja. Asubuhi ilipokwisha na Godfrey kumuaga kwamba anakwenda kuonana na wafanyabiashara wenzake kikaoni, akaanza kuwasiliana na Bwana Saed na kumwambia kwamba alikuwa na muda, kama alikuwa na nafasi waonane katika hoteli yoyote ile.
“Unapafahamu Bavaria?” aliuliza Bwana Saed.
“Ndiyo!”
“Nenda hapo! Ukifika, waambie kwamba wewe ni mgeni wangu, utapewa chumba na nitakuja huko! Nina kikao kidogo na wafanyabiashara wenzangu!” alisema Bwana Saed kwenye simu.
“Sawa mpenzi! Ila unajua malipo yake?”
“Niliambiwa ni dola elfu moja!”
“Ndiyo mpenzi!”
“Nitakupa dola elfu tano! Kwani nimeangalia picha zako, zimenidatisha kishenzi!” alisema Saed maneno yaliyomfanya Fareed kutoa tabasamu pana.
Hakutaka kuchelewa, akaondoka hotelini hapo na kuelekea katika hoteli aliyokuwa ameambiwa. Njiani, bado alijiona kuwa na uhitaji mkubwa wa kutafuta pesa. Alijua kwamba alikuwa akijidhalilisha lakini hakutaka kujali, alijitoa, hayo ndiyo yalikuwa maisha yake ya kila siku, alikuwa tayari kuutumia mwili wake kwa staili yoyote ya maisha lakini mwisho wa siku apate pesa.
Hakuchukua dakika nyingi akafika katika Hoteli ya Bavaria, akateremka kutoka kwenye teksi na kisha kumlipa dereva na kuanza kuelekea ndani. Mavazi yake, kwa kumwangalia ingekuwa vigumu kugundua kama alikuwa mwanaume, alijiremba na kujiremba, hata kutembea kwake alitembea kwa mikogo huku akijitingisha kwa nyuma.
“Nimekuja kumuona Bwana Saed,” alisema Fareed kwa sauti ya kike.
“Sawa. Nenda chumba namba 18,” alisema msichana wa mapokezi huku akimpa ufunguo wa chumba hicho.
Akaupokea na kuanza kuelekea huko. Moyo wake ulikuwa kwenye furaha tele, aliamini kwamba kama siku hiyo angepewa kiasi cha dolaa elfu tano kingekuwa kiasi kikubwa sana ambacho angefanya mambo mengi sana katika maisha yake.
Alipofika ndani ya chumba hicho, akajilaza kitandani na kuanza kumsubiri mwanaume huyo kwa hamu kubwa. Hakutulia pale chumbani, wakati mwingine alikuwa akisimama na kuanza kutembeatembea huku na kule, wakati mwingine alikwenda bafuni na kisha kuanza kujiangalia kwenye kioo.
Aliibinua midomo yake, alijiweka vilivyo, akajiosha, akaona hiyo haitoshi, akaoga kabisa na kujipulizia manukato ya Zenji kama kawaida yake.
Aliporudi chumbani, akachukua simu yake na kumtumia ujumbe mfupi Bwana Saed kwa kumwambia kuwa alikuwa tayari na ni yeye tu ndiye aliyekuwa akimsubiri.
“Nipo tayari! Nakusubiri wewe mume wangu! Mbona unakawia! Jamani utaniua kwa presha!” aliandika ujumbe huo na kumtumia.
Bwana Saed aliupata ujumbe huo, pale alipokuwa kwenye kikao, akaachia tabasamu pana. Moyo wake ukajisikia raha kupita kawaida, akawaangalia wenzake walikuwa kwenye kile kikaona na kuona kama walikuwa wakimpotezea muda.
Kwenye kikao hicho pia alikuwepo Godfrey. Macho yake yalikuwa yakimwangalia Bwana Saed, hakujua ni kitu gani alikiona kwenye simu yake mpaka kuonekana kuwa na furaha kiasi hicho, hakutaka kumfuatilia sana, akajua mambo yake, akafuatilia kikao kile mpaka kilipokwisha.
Bwana Saed hakutaka kubaki mahali hapo, haraka sana akaondoka kwa kuwaaga wachache, alihisi kama angeendelea kubaki mahali hapo basi Fareed angekasirika na kuondoka zake.
Alipofika nje, akamwambia dereva wake kwamba alitakiwa kuendesha gari kwa mwendo wa kasi kuelekea katika Hoteli ya Bavaria. Safari hiyo iliwachukue dakika tano tu, walipofika, akaelekea huko chumbani na kumkuta Fareed akiwa kitandani.
“Nimekuja harakaharaka kama nimepaa,” alisema Bwana Saed huku akivua koti lake na kumfuata Fareed pale alipokaa.
****
Akili ya Godfrey ilikuwa ikimfikiria Fareed tu, kila alipokaa, kichwa chake kilikuwa kwa mwanaume huyo tata. Kikaoni hakuwa na furaha, kila alipokaa alikuwa akimfikiria kiasi kwamba wakati mwingine alijiona kama mgonjwa kwa jinsi aliyokuwa amechanganyikiwa kwa penzi lake.
Siku hiyo hali ilionekana kuwa tofauti kabisa, kila alipokuwa, mara kwa mara alikuwa akisumbuliwa na Fareed kwa kutumiwa meseji na hata wakati mwingine video lakini siku hiyo, alikaa mwanzo wa kikao mpaka mwisho hakukuwa na meseji yoyote aliyokuwa ametumiwa.
Akahisi kwamba kuna tatizo, akahisi kwamba Fareed alikuwa na mwanaume mwingine, moyo wake uliumia, ukamchoma kupita kawaida, hakutaka kukubali, akaanza kumpigia simu, cha ajabu simu ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
“Mbona hapokei simu? Kuna nini? Au yupo na mwanaume mwingine? Au kuna mwenzangu kamuona akirandaranda akamteka, hapana! Ni lazima niwahi kurudi,” alisema Fareed huku akionekana kuchanganyikiwa hasa.
Hakukuwa na raha kikaoni hapo, muda wote kichwa chake kilivurugika, kwa kile kilichokuwa kimetokea cha kutokutumiwa meseji kiliuchanganya moyo wake, hivyo alipotoka kikaoni, moja kwa moja akaingia ndani ya gari alilolikodi kulitumia na kurudi hotelini.
Hakuchukua muda mrefu, akafika na moja kwa moja kuteremka na kuanza kuelekea humo. Alikimbia kama mtu aliyekuwa na haraka fulani, alipoingia ndani ya chumba hicho, hakumuona Fareed, akaelekea bafuni, napo hakuwepo na kila alipompigia simu, iliita bila kupokelewa, uso wake ukavimba kwa hasira.
“Huyu malaya atakuwa ananisaliti! Atakuwa amelala na mwanaume mwingine,” alijisemea huku akionekana kuwa na hasira kali mno.
Aliendelea kumpigia simu, haikuwa ikipokelewa na mwisho wa siku kutokupatikana kabisa, alichanganyikiwa na moyo wake kujawa na hasira kali.
Muda ulizidi kusogea, ilikuwa asubuhi, mchana ukaingia, alasiri nayo ikasogea na kukatika, jioni ikaondoka, ilipofika usiku wa saa 2:03 akasimama dirishani, kwa kule juu, akaona teksi ikiingia na kwa mbali akamuona Fareed akiteremka huku akiwa na mkoba wake alioubeba kama mwanamke.
Godfrey akapandwa na hasira zaidi, akavua suruali yake, akachomoa mkanda, usiku huo, hakutaka kusikia kitu chochote, moyo wake uliwaka kwa hasira, akasimama huku akitetemeka, mkanda mkononi, mara Fareed akaufungua mlango na kuingia ndani ya chumba hicho. Hali aliyomkuta nayo Godfrey ilimshtua, akakiona kifo mbele yake.
***
Fareed alibaki akimwangalia Godfrey, aliogopa, jinsi mwanaume huyo alivyovimba ilionyesha dhahiri kwamba angeweza kumpiga hapo chumbani. Alibaki akitetemeka lakini akajipa moyo kwamba angeweza kufanya lolote liwezekanalo kuupoza moyo wa mwanaume huyo uliokuwa na hasira kali.
“Bebi kuna nini?” aliuliza Fareed kwa sauti ndogo, sauti ya kike ambayo ilipenya moja kwa moja mpaka moyoni mwa Godfrey na kuutetemesha mtima wa moyo wake.
Wakati akiwa ameuliza swali hilo, Fareed alimsogelea Godfrey na kisha kuushika mkono wake, hakuridhika, akauweka mkono wake mwingine katika kifua cha mwanaume huyo.
Hasira zote alizokuwa nazo Godfrey zikaanza kupotea, hakuamini kama kweli Fareed angeweza kuzimaliza hasira kali alizokuwa nazo kirahisi namna hiyo. Moyo wake ukarudi ndani ya penzi zito, kila alipomwangalia akahisi kabisa kuwa na mapenzi mazito na Fareed hivyo kujikuta mkono wake ukilainika na kuudondosha mkanda aliokuwa ameushika.
“Kuna nini my love jamani! Mbona unanitisha?” aliuliza Fareed huku akiuhamishia mkono wake na kuanza kukishikashika kidevu chake.
“Umetoka wapi jamani?” aliuliza Godfrey, alilainika kirahisi sana kiasi kwamba hata yeye mwenyewe hakutegemea.
“Nilikuwa nimekwenda kutembea!”
“Ndiyo mpaka usiku!”
“Naomba unisamehe baba watoto,” alisema Fareed kwa sauti iliyoutetemesha moyo wa Godfrey kupita kawaida.
Hakutaka kuendelea kulalamika, akamvuta na kukaa kitandani. Muda wote huyo Fareed alikuwa akimwangalia Godfrey, alimpenda lakini hakuona kama mwanaume huyo alikuwa na uwezo wa kumzuia asifanye mambo yake kwani katika maisha yake hakuwa akitegemea mwanaume mmoja, alikuwa akiishi maisha ya kutegemea wanaume wengi.
“Hutoniweza. Mimi ni popo, naruka popote nipatakapo,” alisema Fareed kwa sauti ya moyoni huku akimwangalia Godfrey ambaye alionekana kuridhika kwa kile alichokuwa akifanyiwa.
***
Kwa jina aliitwa Asteria Kimaro, alikuwa mwanamke mtu mzima aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa jijini Dar es Salaam. Alikuwa na maduka mengi ya vipodozi, alikuwa akimiliki biashara nyingi ambazo zilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha.
Japokuwa alikuwa akifanya biashara ya halali lakini upande mwingine alikuwa akifanya biashara ya magendo. Kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwachukua wanawake kwa kisingizio cha kuwapeleka nchi mbalimbali kufanya kazi lakini mwisho wa siku alikuwa akiwauza na kuwafanyisha biashara za ngono.
Mbali na wasichana hao lakini pia kulikuwa na wengine waliokuwa wakiishi nchini Tanzania lakini kila walipokuwa wakihitajika kingono nje ya nchi, alikuwa akipigiwa simu na kuambiwa, kiasi cha fedha alichokuwa akilipwa msichana husika, na yeye alichukua chake.
Biashara hiyo ilikuwa kubwa, ilimuingizia kiasi kikubwa cha fedha. Kila siku wanawake waliendelea kujiandikisha kwake na walipotokea wanaume, walisafirishwa na kuelekea nje ya nchi kwa ajili ya ngono tu.
Hakutaka kuishia kwa wanawake bali akapanua biashara yake na kuwachukua wanaume tata na kuanza kuwasafirisha kwenda huko. Biashara hiyo ilikuwa kubwa kwa nchi za Uarabuni kwa kuwa kulikuwa na wanaume wengi waliokuwa wakitamani mapenzi ya jinsia moja hivyo alijizatiti sasa katika nchi hiyo.
Katika biashara hiyo ndipo alipokutana na Fareed. Siku ya kwanza kumuona yeye mwenyewe alishtuka. Aliwaona wanaume wengi wa aina hiyo lakini si kama alivyokuwa Fareed.
Alikuwa mzuri wa sura, msafi, mwenye umbo maridhawa na sauti ya kuvutia. Alipoambiwa kwamba na huyo alikuwa mmoja wa wanaume tata waliotaka awe wakala wake, alichanganyikiwa kwani aliamini kwamba angepata kiasi kikubwa cha fedha kama tu angekubaliana naye na kuingia mkataba.
Wakakaa chini na kuzungumza, halikuwa tatizo, alitaka kupanua biashara yake hivyo akasaini naye mkataba na ndiye alikuwa mtu wa kwanza kufikiriwa kila dili la nje lilipokuwa likifika mezani kwake.
Akaanza kumnadi kwa wateja wake, akawatumia picha kwa kuwaambia kwamba mali mpya iliwasili, kila aliyemuona, alichanganyikiwa, hawakuamini kama kungekuwa na mtoto mashalaah kama alivyokuwa Fareed.
“How much?” (kiasi gani?) aliuliza mwanaume aliyekuwa akiishi Qatar.
“Three thousand dollars?” (dola elfu tatu)
“I want her,” (namuhitaji)
Hiyo ndiyo biashara iliyokuwa ikifanyika, Asteria aliendelea kutengeneza utajiri, serikali haikumgundua kile alichokuwa akikifanya. Wale waliopata hela, wakawaambia wenzao na hatimaye idadi ya wanaume tata ikazidi kuongezeka nchini Tanzania, hasa katika Jiji la Dar es Salaam.
Asteria aliijua biashara ya uwakala, alijitoa, alihangaika huku na kule kuwatafuta wateja, alikuwa akiwapata na malipo kufanyika. Mpaka kipindi hicho, Fareed alikuwa amekwenda nchini nyingi, hasa za Uarabuni ambapo matendo hayo yalishamiri kwa kiasi kikubwa sana.
Baada ya miezi kadhaa, Asteria akampata bilionea Saed na kumwambia kuhusu Fareed. Mwarabu huyo alichanganyikiwa zaidi baada ya kutumiwa picha. Akapata uroho, udenda ukamtoka na kuhitaji kuwasiliana naye.
Walifanya yao na siku chache mbele, wakala huyo akapokea simu kutoka nchini Marekani, kwa Bilionea Cotton Keith ambaye alimwambia kwamba alisikia mambo mengi kuhusu yeye hivyo alihitaji msichana.
“Msichana?” aliuliza Bi Asteria.
“Ndiyo!”
“Sawa. Una dola elfu tano?”
“Swali la kitoto sana hilo. Unajua unazungumza na nani?” aliuliza bilionea huyo.
“Hapana!”
“Hebu angalia Google jina la Cotton Keith,” alisikika mwanaume huyo na kukata simu.
Asteria akakata simu na kisha kufanya kama alivyoambiwa. Hakuamini macho yake baada ya kugundua kwamba alikuwa akiwasiliana na bilionea mkubwa nchini Marekani. Kwanza akaanza kutetemeka, yeye mwenyewe alihofu, hakujiamini kwani miongoni mwa watu waliokuwa mabilionea, Keith alikuwa balaa.
“Umeona sasa?” aliuliza Keith baada ya kumpigia simu.
“Ndiyo! Unahitaji wanawake wangapi?”
“Tuanze na mmoja.”
“Nitakupa aitwaye Penny?”
“Anajua?”
“Usiwe na shaka na watu wangu. Wewe niachie anuani yako!” alisema Asteria na kukata simu.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kufahamiana na bilionea huyo, mara kwa mara walikuwa wakiwasiliana huku akimwambia kwamba alikuwa akihitaji wanawake zaidi. Alipenda kufanya ngono na wanawake weusi, maishani mwake, japokuwa alikuwa Mzungu lakini hakuwapenda Wazungu.
Wakatengeneza uswahiba mkubwa na kujikuta ndani ya miezi sita wakiwa marafiki wakubwa. Wakati mwingine Asteria alikuwa akisafiri mpaka nchini Marekani ambapo huko alikutana na mwanaume huyo na kuzungumza mambo mengi.
Biashara yake iliendelea kukua. Alizidi kuwasafirisha wanawake kwenda huko kwa ajili ya kufanya nao mapenzi na bilionea huyo.
Baada ya mwaka mmoja kupita huku urafiki wao ukiwa mkubwa ndipo siku moja bilionea huyo akamualika Asteria katika shere yake ya kuzaliwa ambayo angeifanya Jijini Los Angeles, alimuomba sana ahudhurie kwani ilikuwa ni sherehe kubwa ambayo ingekutanisha mastaa wengi kutoka sehemu mbalimbali hapo Marekani.
“Nitakuja!”
“Njoo na marafiki zangu basi!”
“Haina shida. Wangapi?”
“Wawili!”
“Sawa.”
Asteria akafurahia, moyo wake ukajua kwamba hiyo ndiyo ilikuwa nafasi ya kutengeneza fedha zaidi. Hakutaka kuiacha nafasi hiyo, alitaka kuhakikisha anaitumia vizuri kuhakikisha kwa mwaka huo anakuwa na kiasi kikubwa cha fedha.
Akawachukua wasichana wawili, Ester na Queen lakini pia akamuongeza na Fareed kwa kuamini kwamba ndani ya sehemu ambayo wangeonana kwa ajili ya sherehe hiyo ingewezekana kabisa kupata mteja mwingine kupitia Fareed.
“Marekani?”
“Ndiyo! Kuna mabwana wa Kizungu, wenye hela zao,” alisema Asteria.
“Basi sawa. Nitakwenda!”
Fareed alifurahi, kwa kipindi kirefu alitamani kufika nchini Marekani, kitendo cha kuambiwa kwamba alitakiwa kwenda huko, moyo wake ukarukaruka na siku hiyo ilipofika, wakaondoka kuelekea huko.
Baada ya saa zaidi ya ishirini, ndege ikaanza kutuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa LAX uliokuwa hapohapo Los Angeles. Walipoteremka, tayari kulikuwa na gari lililokuwa likiwasubiria ambapo moja kwa moja wakaingia na kuanza kupelekwa katika hoteli waliyotakiwa kufikia.
Njiani, Fareed alikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli alifika Marekani. Aliangalia nje, jinsi jiji hilo lilivyokuwa limejengeka, lilipendeza machoni mwake na kila alipokuwa akiliangalia, alijiona kama yupo katika pepo ndogo.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika hotelini. Wakateremka na kuelekea ndani, huko, wakatulia vyumbani na kuagiza chakula ambapo wakaletewa kwani kila kitu kililipiwa na Bilionea Keith.
“Vipi? Mmekwishafika?” aliuliza bilionea huyo.
“Yeah! Ndiyo tumeingia!”
“Nakuja!”
Wala hazikupita dakika nyingi bilionea huyo akafika hotelini humo na moja kwa moja kuelekea katika chumba hicho. Alipofika katika korido ya iliyokuwa na chumba kile akaingia ndani. Macho yake yakatua kwa watu waliokuwa humo ndani, walikuwa wasichana wazuri, aliwapenda lakini mbali na wasichana hao, alipomwangalia Fareed, akashtuka sana, hakuamini kama kulikuwa na msichana mwingine mzuri namna hiyo.
“Ooh! Ni wasichana wazuri! Naona umeniongezea wa tatu kabisa,” alisema Bilionea Keith huku akitoa tabasamu pana.
Asteria hakujibu, akamvutia pembeni na kuanza kuzungumza naye kuhusu Fareed kwamba hakuwa msichana kama alivyohisi bali alikuwa mwanaume tata maneno yaliyomfanya bilionea huyo kushangaa.
Hakuamini kama kulikuwa na mwanaume aliyekuwa mrembo kama Fareed. Aliwafahamu wanaume tata waliokuwa nchini Marekani, hawakuwa na uzuri mkubwa lakini kwa Fareed alionekana kuwa tofauti, alikuwa na muonekano wa kike na hata maringo yake, jinsi alivyokuwa akiuweka mwili wake, alionekana kama msichana.
“Ni mwanaume?”
“Ndiyo!”
“Unanitania!”
“Siwezi kukutania!”
“Mbona kama mwanamke mrembo?”
“Ndiyo hivyo! Ni mwanaume huyo.”
Bilionea Keith hakuamini, alimwangalia vizuri Fareed, ilikuwa vigumu kufahamu kama mtu huyo alikuwa mwanaume, alionekana kukamilika kama mwanamke kamili. Hakutaka kumganda sana, akaendelea kufanya mambo yake na usiku wa siku iliyofauata, sherehe ikaanza kufanyika katika ukumbi wa Hoteli hiyo.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa wawili hao kuonana, wakabadilishana namba za simu na kuanza kuwasiliana. Bilionea Keith hakuwa na hofu na Fareed, kwake alikuwa rafiki yake mkubwa, alimsaidia kama rafiki yake na wakati mwingine alimuita mpaka Marekani kwa ajili ya kumtembelea.
Hakufanya naye kitu, kila alipokuwa akimuhoji kwa lengo la kutaka kujua mambo mengi zaidi, hasa kuhusu uhusiano, mwanaume huyo hakumficha, alimwambia kwamba alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine aliyeitwa kwa jina la Godfrey.
“Ni mwanaume mwenye bahati sana,” alisema Keith.
“Kwa nini?”
“Kumpata mrembo kama wewe.”
“Kwani mimi mrembo?”
Itaendelea kesho.