IBRAHIM Ajibu yupo kwenye majanga makubwa ndani ya Simba kwa kuhofia kushindwa kuvunja rekodi yake aliyoiweka msimu uliopita alipokuwa anaitumikia Yanga. Rekodi hiyo ni ile ya kutoa asisti nyingi ndani ya msimu mmoja.
Ajibu alipokuwa Yanga msimu wa 2018/19, alitoa asisti 17 na kufunga mabao sita ndani ya Ligi Kuu Bara, huku bao lake la staili ya kubinuka mbele ya Mbao FC likiwa ni bao bora la msimu huo.
Mpaka sasa Ajibu akiwa ndani ya Simba inayoongoza ligi ikiwa imecheza mechi 28, ametoa asisti nne na kufunga bao moja mbele ya Polisi Tanzania. Bado ana deni la asisti 13 kuifikia rekodi yake.
Ajibu ambaye Yanga alikuwa anavaa kitambaa cha unahodha, akiwa Simba msimu huu amecheza mechi 16 kati ya 28 za ligi kuu. Katika mechi hizo, ametumia dakika 705 akiwa na wastani wa kutoa asisti kila baada ya dakika 176 ambapo alitoa kwa Miraji Athuman, Sharaf Shiboub, Clatous Chama na Jonas Mkude.
Kutokuwa na uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza, ndiyo sababu ya kiungo huyo mshambuliaji kusotea rekodi yake hiyo.
STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA, DAR

