MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amefunguka kuwa wamebaini kuwepo kwa kamati za chinichini kutoka kwa wapinzani wao Simba wanaotaka timu yao ipoteze kwenye kila mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao watacheza.
Mwakalebela amesema wamekuwa wakipata taarifa juu ya kamati zilizoundwa katika Jiji la Dar zikiongozwa na baadhi ya viongozi wa Serikali ambao wanataka kuirudisha nyuma klabu yao, huku akifunguka zaidi yapo mengi ambayo wameyahifadhi moyoni ambapo wakiamua kuyasema, amani itatoweka.
Akizungumzia ishu hiyo, Mwakalebela alienda mbali akisema, wapo watu ambao tayari walitangulia mkoani Lindi, wakati wanajiandaa na mchezo wao wa jana dhidi ya Namungo, ambapo lengo lao kubwa ni kutengeneza mazingira ili tu Yanga iweze kufungwa kwa idadi kubwa ya mabao, jambo ambalo wao walishalishtukia.
“Uongozi wa Yanga umekuwa ukipokea taarifa mbalimbali juu ya vitendo vya baadhi ya watu kuunda makundi yakiongozwa na baadhi ya viongozi wakiwekeza nguvu zao katika kuirudisha nyuma klabu yetu, tumepokea taarifa za vitendo vya hujuma ambavyo vinaendelea kule Namungo kuelekea katika mchezo wetu wa leo (juzi Jumapili).
“Kwa hiyo mimi niseme kwamba, vitendo hivyo tumeshavijua, tunachosubiri tuone kama timu yetu itakuwa haitendewi haki uwanjani kwa
maana ya ‘Fairness’, kama ikitokea tumeonewa sisi hatutakubali, tutatoka mbele na kuipigania haki yetu, kwa sababu tuna mambo mengi sana moyoni, lakini tumekosa pa kuyasemea,” alisema Mwakalebela.
Ofisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, mara kadhaa amekuwa akisema kuwa bila makandokando Yanga haifungwi.
Walipotafutwa Simba kuzungumzia tuhuma hizo jana, Meneja wa klabu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema: “Hizo ni habari za kipuuzi, ambazo sisi kama Simba hatuwezi kuzifanya. Tunaongoza ligi kwa tofauti ya pointi 15, sasa tuwahujumu Yanga kwa shida gani? Kwanza mimi kama kiongozi siwezi kuzungumzia hivyo vutu kabisa kwa sababu havina maana.”
ISSA LIPONDA, Dar es Salaam
