×

STAMICO Yanunua Mitambo Ya Kisasa Zaidi Kuwahi Kutokea Nchini

Katibu Mkuu wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mitambo mitatu ya kisasa kutoka Stamico, kulia ni Mkurugenzi wa Stamico, Dkt. Venance Mwasse.

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limenunua mitambo mitatu ya uchorongaji yenye teknolojia ya kisasa zaidi kuwahi kutumika hapa nchini.

Mitambo hiyo iliyonunuliwa kwa thamani ya Sh bilioni 5.2, kati ya mitambo hiyo mitatu mmoja  una uwezo wa kuendeshwa kwa kutumia kompyuta na mtu akiwa mbali na mashine ili kulinda usalama wake na wa mazingira.

Akizungumza katika uzinduzi wa mitambo hiyo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila ameipongeza STAMICO kwa hatua kubwa waliyofikia na uthubutu wa kuleta ushindani katika soko la uchorongaji nchini.

Wadau wakiiangalia mitambo hiyo.

Pia amewataka STAMICO kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuleta tija na maendeleo kwa taifa.

“Matunda haya yametokana na ufanisi wa STAMICO, mmeweza kutumia rasilimali zenu na leo mmenunua mitambo ya mabilioni ya shilingi, tunatambua utafiti katika migodi mikubwa nchini ulifanywa na STAMICO huko nyuma, sasa mna zabuni za kwenda kuchoronga kwenye migodi hivyo na ninyi mtafute leseni muanzishe migodi yenu wenyewe.

“Mna mgodi wa Stamigold na Kiwira ambayo inafanya vizuri lakini muende mbele zaidi ili siku moja tukitaja mgodi mkubwa wa dhahabu uwe unamilikiwa na Stamigold,” alisema.

Akizungumzia kuhusu mitambo hiyo, Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse alisema ni jambo la kujivunia kununua mitambo hiyo ya kisasa.

Alisema mitambo hiyo imenunuliwa kutoka Kampuni za Epiroc (Sweden) na Son-mak (Uturuki).

“Tumenunua mitambo hii mitatu ya kisasa kabisa na mmoja kati ya huo mtambo ni Explorac 235 wenye uwezo wa kuchimba hadi mita 500 kwenda chini lakini kwenye sekta ya madini hapa nchini makampuni yana mitambo ya kuchimba mita 300 pekee.

“Ni Stamico pekee wenye mtambo huu ambao una uwezo wa kuchimba mita 200 kwa siku, wengine kwenye sekta hii mitambo yao ina uwezo wa kuchimba mita 100 hadi 150 kwa siku,” alisema.

Ameendelea kusema kuwa mitambo hiyo ya kisasa ni salama kwa mazingira kwa sababu hata wasimamizi hawatapigwa vumbi.

Katibu Mkuu akiwa kwenye pozi la kushangilia baada ya uzinduzi huo.

“Mtambo huu ni mpya na teknolojia yake ni ya hali ya juu kwa sababu hakuna kampuni nyingine ambayo imeshawahi kutumia mtambo wa aina hii hapa nchini. STAMICO ndio shirika la kwanza kuwa na mtambo kama huu,” alisema.

Dkt. Mwasse ameishukuru wizara ya madini kwa maelekezo na ushirikiano unaoendelea kutolewa kwa STAMICO na kutoa rai kwa wadau wadau wa uchorongaji kufanya kazi na STAMICO.

Alisema mitambo hii inategemea kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali tayari kuanza kazi ya uchorogaji mara moja.

Katibu Mkuu wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dkt. Venance Mwasse (kulia), wakishangilia baada ya kuzindua mitambo hiyo.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Epiroc, Menas Ngonyani aliishuku Stamico kwa kuwaamini na kuagiza mitambo hiyo ambayo ni ya kisasa zaidi nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Son-mak,  Joseph Mbunda alisema Stamico imekuwa ikifanya kazi na kampuni hiyo tangu ilipoingia nchini mwaka 2004.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (kushoto) akimpongeza Mkurugenzi wa Stamico, Dkt. Venance Mwasse (kulia), baada ya kuzindua mitambo mitatu ya kisasa ya kuchoronga.

“Stamico wamekuwa wateja wetu wakubwa, tunashukuru sana kwa kutuamini, na tunawahakikisha kuwaletea mitambo imara, ya kisasa yenye ufanisi ili kukuza sekta ya madini nchini” alimaliza kusema.

Leave a Comment