
MBUNGE wa Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Mwangika, Kata ya Bangwe, ambapo amesikiliza kero zao live ikiwemo tatizo la maji.
Wakizungumza wakati wa mkutano huo, akina mama wa Mwangika wamemtaka mbunge huyo awatue ndoo kichwani kwani ndoa zao zimekuwa matatani kwa sababu ya kuchelewa kurudi nyumbani wakitafuta maji safi na salama kwa ajili ya familia zao.
“Waheshimiwa mbunge na diwani wetu, sisi akina mama wa Mwangika tunayo kero moja kubwa ya kupata maji safi, hili limekuwa tatizo sugu hapa kijijini kwetu, ndoa zetu zimekuwa hazina amani, tukichelewa tunapigwa na waume zetu kwa sababu ya maji. Tunaomba sana utusaidie kututua ndoo kichani, tunateseka mno,” amesema Bi. Nyagaya Kasika Malima.
Akitatua kero hiyo, Mhe. Shigongo alimpigia simu live meneja wa maji Sengerema ambaye alisema kuwa kuna mradi mkubwa wa maji utaanza kutekelezwa hivi karibuni katika eneo hilo, ambao ukikamilika utahudumia vijiji vya Bupandwamhela, Mwangika mpaka Kahunda na maeneo ya jirani na vijiji hivyo.