×

Biashara Kufanya Usajili wa Kibabe CAF

BIASHARA United imesema kuwa, kuelekea michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), imepanga kufanya usajili mkubwa ambao utawawezesha kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

 

Timu hiyo yenye makazi yake Musoma mkoani Mara, imepata nafasi hiyo baada ya kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu, huku CAF ikiipa Tanzania nafasi nne za klabu zake kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Akizungumza na Spoti Xtra, Katibu Mkuu wa Biashara United, Haji Mtete, alifunguka kwamba: “Tunamshukuru Mungu malengo ambayo tulijiwekea tumeyafikia kwani moja ya malengo hayo ni kuhakikisha msimu huu tunamaliza kwenye nafasi nne za juu jambo ambalo tumelifanikisha kwa ukubwa wake.

 

“Kwa sasa tumejikita kuanza maandalizi kuelekea michuano ya kimataifa, kwa kufanya maboresho kadhaa kwenye kikosi chetu kwa kusajili wachezaji bora ili kuleta ushindani kwenye michuano hiyo na kuzilinda nafasi nne ambazo Tanzania tunazo.”

Leave a Comment