×

Waleteni…. Kisinda Apata Leseni Ya Caf Kucheza na Al Hilal ya Nchini Sudan

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Tuisila Kisinda.

 

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Tuisila Kisinda, sasa ni ruksa kuichezea timu hiyo katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara baada ya juzi kupata leseni kutoka Caf.

 

Staa huyo ni kati ya wachezaji waliosajiliwa na timu hiyo, katika msimu huu ambaye amekuja kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya Yanga.

 

Kisinda amejiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Klabu ya RS Berkane ya nchini Morocco.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwenyekiti wa Mashindano wa Yanga, Rogers Gumbo, alisema kuwa kiungo huyo ataanza kuonekana katika michuano ya kimataifa katika raundi ya kwanza watakayokutana na Al Hilal ya nchini Sudan.

 

Gumbo alisema kuwa kiungo huyo leseni yake ilitoka Caf juzi Ijumaa, hivyo ruksa kuanza kucheza katika hatua hiyo inayofuatia mara baada ya kufuzu kutokea ile ya awali.

 

Aliongeza kuwa uwepo wa kiungo huyo katika hatua hiyo inayofuatia utaimarisha kikosi chao kufanya vema katika mashindano hayo makubwa Afrika.

 

“Kisinda atacheza kimataifa, lakini ataanzia raundi ijayo mara baada ya raundi hii dhidi ya Zalan kumalizika kwa kuwaondoa katika mashindano haya makubwa Afrika.

 

“Ni baada ta kupata leseni yake ambayo imetoka juzi Ijumaa baada ya kumuingiza kwenye usajili wa kimataifa wa Caf, kwa hiyo atacheza kimataifa kuanzia raundi ijayo,” alisema Gumbo.

STORI: WILBERT MOLANDI

Leave a Comment