
Rais Samia Suluhu Hassan leo, Oktoba 22, 2023, amemteua Sophia Mjema kuwa mshauri wa rais wa masuala ya wanawake na makundi maalum ambapo kabla ya uteuzi huo, Mjema alikuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM.
Kuteuliwa kwa Mjema kuwa Mshauri wa Rais, kunaifanya nafasi aliyokuwa akiishikilia, ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kuwa wazi, jambo ambalo limeanza kuamsha gumzo miongoni mwa wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini, wakijaribu kuhoji ni nani atakayekuwa mrithi wa nafasi hiyo?
Kabla ya Mjema kushika wadhifa wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Shaka Hamdu Shaka ambaye naye alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Humphrey Polepole ambaye alirithi mikoba ya Nape Nnauye katika nafasi hiyo.
Je, nani anakwenda kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, hasa katika kipindi hiki ambacho joto la uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 limeanza kupanda? Muda utazungumza.