Uganda Yasimamisha Mashirika 10 ya Kiraia Siku Moja Kabla ya Uchaguzi

Serikali ya Uganda imeamua kusitisha kwa muda usiojulikana shughuli za mashirika 10 yasiyo ya kiserikali (NGOs), ikieleza kuwa uamuzi huo umetokana na sababu za kiusalama na kisheria.
Mashirika yaliyosimamishwa ni pamoja na Jukwaa la Kitaifa la Mashirika ya Kiraia (National NGO Forum), Chapter Four Uganda, Alliance for Election Finance Monitoring (ACFIM), Human Rights Network for Journalists–Uganda (HRNJ-U), na National Coalition of Human Rights Defenders in Uganda (NCHRD-U).
Hatua hiyo imechukuliwa siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho, Alhamisi Januari 15, 2026, hatua ambayo imezua mjadala mpana ndani na nje ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumanne, Januari 13, 2026, na Ofisi ya Kitaifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Uganda (National Bureau for NGOs), mashirika hayo yamesimamishwa ili kutoa nafasi kwa uchunguzi kuhusu shughuli zao.
Mtandao wa Nation Africa umeripoti kuwa ofisi hiyo imedai kupokea taarifa za kijasusi zinazoonyesha kuwa baadhi ya mashirika hayo yalijihusisha na shughuli zinazokiuka au kuhatarisha sheria za Uganda.
Kutokana na taarifa hizo, ofisi hiyo imeamuru mashirika husika kusitisha shughuli zao kwa muda usiojulikana, huku ikieleza kuwa uchunguzi unaoendelea utaamua hatima ya mashirika hayo. Hata hivyo, haikutoa maelezo ya kina kuhusu tuhuma zinazoyakabili mashirika hayo.
Stori na Elvan Stambuli, Global Digital

