×

Bajeti Kuu ya Serikali kugusa maeneo muhimu ya kiuchumi

 

Siku moja kabla ya kusomwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imeeleza kuwa bajeti hiyo inalenga kujenga uchumi himilivu kupitia mageuzi ya kidijitali, uwekezaji wa kimkakati na sera endelevu za kibajeti kwa ukuaji jumuishi wa uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 10, 2026, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema bajeti ya mwaka 2026/27 ni ya kwanza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na imeandaliwa kwa kuzingatia Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025.

Katika maandalizi ya bajeti hiyo itakayosomwa kesho Alhamisi Juni 11, 2026 Serikali imepokea mapendekezo 727 kutoka kwa wadau wa Serikali na sekta binafsi kuhusu maboresho ya kodi, ada na tozo mbalimbali.

Mapendekezo hayo yalifanyiwa uchambuzi na Kamati ya Wataalam ya Maboresho ya Kodi pamoja na Kamati ya Kiufundi ya ngazi ya juu, ambapo maoni na ushauri vimezingatiwa katika mapendekezo yatakayowasilishwa Bungeni.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, bajeti ya mwaka 2026/2027 itakuwa na mwelekeo wa kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia maboresho yatakayostawisha sekta mbalimbali za uzalishaji, kuongeza mapato ya ndani ya Serikali ili kuimarisha uwezo wa nchi kujitegemea kibajeti, pamoja na kuimarisha nidhamu katika matumizi ya fedha za umma.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa bajeti hiyo itaweka msisitizo katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala, kuongeza kasi ya urasimishaji wa sekta isiyo rasmi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini, pamoja na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kufanya malipo ili kupunguza utegemezi wa fedha taslimu.

Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa itaendelea kuimarisha ushirikishwaji wa wadau na wananchi katika maboresho ya mfumo wa kodi na sera mbalimbali za kiuchumi kwa lengo la kuhakikisha kuwa bajeti inayotekelezwa inawanufaisha wananchi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Hatua mahsusi na maelezo ya kina kuhusu mapato, matumizi na maboresho mbalimbali ya sera yatatangazwa rasmi wakati wa uwasilishaji wa Bajeti Kuu ya Serikali.

 

Leave a Comment