
Mahakama ya Rufaa ya Tanzania leo, Julai 3, 2026, inatarajiwa kusikiliza maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi ya Tundu Lissu kuhusu mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili.
Maombi hayo yenye namba 7440840 ya mwaka 2026 yatasikilizwa na Jopo la Majaji watatu. Kutokana na ukumbi wa Mahakama ya Rufaa kuwa na nafasi ndogo, usikilizwaji wa shauri umehamishiwa katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Katika shauri hilo, Lissu anatarajiwa kuwasilisha hoja zake za kisheria mbele ya jopo hilo la majaji, huku Serikali kupitia DPP ikiendelea kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliokataa ombi la kuruhusu kuwasilishwa kwa ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Jamhuri iliwasilisha maombi hayo ya mapitio Februari 24, 2026, ikiitaka Mahakama ya Rufaa ipitie uamuzi wa Mahakama Kuu uliokataa ombi la kuwasilisha ushahidi huo wa ziada.
Shauri la mapitio namba 7203216/2026 linasikilizwa na jopo linaloongozwa na Augustine Mwarija, akisaidiana na Zainabu Muruke na Amour Khamis.
Awali, shauri hilo lilikuwa limepangwa kusikilizwa Juni 11, 2026, lakini liliahirishwa hadi Julai 3, 2026 bila sababu za kuahirishwa huko kuwekwa wazi.
Kesi hiyo inaendelea kuvutia ufuatiliaji mkubwa kutokana na uzito wa mashtaka yanayomkabili Mwenyekiti huyo wa CHADEMA na athari zake katika mjadala wa kisiasa na kisheria nchini.