
Kylian Mbappe ameandika historia mpya katika Kombe la Dunia baada ya kumpita Lionel Messi na kuwa mfungaji bora wa muda wote katika historia ya mashindano hayo.
Nyota huyo wa Ufaransa alifunga mabao mawili katika mchezo wa kusaka mshindi wa nafasi ya tatu dhidi ya England uliochezwa Jumamosi mjini Miami Gardens, na kufikisha jumla ya mabao 22 katika historia ya Kombe la Dunia, akimpita Messi aliyekuwa na mabao 21.
Mbappe alifunga bao lake la kwanza dakika ya 48 kwa shuti lililompita kipa Dean Henderson, wakati bao la pili alilifunga dakika ya 66 kwa shuti la mguu wa kushoto kutoka ndani ya eneo la hatari.

Mabao hayo yalisaidia Ufaransa kupunguza pengo kutoka mabao 4-0 hadi 4-3, ingawa hatimaye England iliibuka na ushindi wa mabao 6-4 na kutwaa nafasi ya tatu.
Mbali na rekodi hiyo, Mbappe sasa anaongoza pia mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu (Golden Boot) akiwa na mabao 10 katika Kombe la Dunia la 2026, mawili zaidi ya Lionel Messi.
Miaka minne iliyopita nchini Qatar, Mbappe alitwaa tuzo hiyo baada ya kufunga mabao nane, licha ya Ufaransa kupoteza fainali dhidi ya Argentina ya Messi kwa mikwaju ya penalti.
Ufaransa ilikosa nafasi ya kucheza fainali ya tatu mfululizo ya Kombe la Dunia baada ya kuondolewa na Hispania katika hatua ya nusu fainali, huku mchezo wa kusaka mshindi wa nafasi ya tatu ukiwa wa heshima zaidi kuliko kuwania taji.