×

Filamu ya The Odyssey Yaingiza Zaidi ya Bilioni 700 Wikiendi ya Kwanza, Yaweka Rekodi Mpya

Filamu mpya ya The Odyssey, iliyoongozwa na mshindi wa Tuzo za Oscar Christopher Nolan, imeanza kwa mafanikio makubwa baada ya kuingiza zaidi ya Shilingi bilioni 713 za Tanzania katika wikiendi yake ya kwanza kuonyeshwa duniani.

Kwa makadirio ya kiwango cha ubadilishaji wa fedha (takribani Shilingi 2,700 kwa dola moja), mapato ya filamu hiyo ya dola milioni 264.1 yanalingana na zaidi ya Shilingi bilioni 713.

Ndani ya Marekani pekee, filamu hiyo imekusanya dola milioni 124.5, sawa na takribani Shilingi bilioni 336, huku masoko ya kimataifa yakichangia dola milioni 139.6, ambazo ni karibu Shilingi bilioni 377.

Mafanikio hayo yanaifanya The Odyssey kuwa filamu yenye ufunguzi wa tatu kwa ukubwa nchini Marekani mwaka 2026, nyuma ya Toy Story 5 na The Super Mario Galaxy Movie. Pia ndiyo filamu iliyompa Christopher Nolan ufunguzi mkubwa zaidi wa kimataifa katika taaluma yake ya uongozaji.

Filamu hiyo ni muendelezo wa kazi ya Nolan baada ya mafanikio ya Oppenheimer, iliyoshinda Tuzo saba za Oscar mwaka 2024.

The Odyssey ni tafsiri ya kisasa ya simulizi maarufu la mshairi wa kale wa Kigiriki Homer, likimfuatilia mfalme wa Ithaca, Odysseus, anayechezwa na Matt Damon, katika safari yake ya miaka 10 ya kurejea nyumbani baada ya vita.

Mbali na Matt Damon, filamu hiyo imewakutanisha nyota wengine wa Hollywood akiwemo Tom Holland, Zendaya, Anne Hathaway na Robert Pattinson.

Hata kabla ya kuonyeshwa rasmi, The Odyssey ilikuwa tayari imeweka rekodi kwa mauzo ya tiketi za maonyesho ya IMAX 70mm, huku baadhi ya tiketi zikiuzwa tena kwa bei ya zaidi ya Shilingi milioni 2.7 (zaidi ya dola 1,000) katika soko la mitandaoni.

Aidha, filamu hiyo imepokelewa vizuri na wakosoaji, ikiwa na alama ya asilimia 96 kwenye tovuti ya Rotten Tomatoes, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa filamu zinazotajwa kuwa bora zaidi kuwahi kuongozwa na Christopher Nolan.

Kwa kasi hii ya mapato, The Odyssey inaonekana kuwa moja ya filamu zitakazotawala soko la sinema duniani mwaka 2026.

Leave a Comment