
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Taifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 yatafanyika kuanzia Agosti 15 hadi 20 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Prof. Mkenda amesema maadhimisho hayo yataongozwa na kaulimbiu isemayo, “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” yenye lengo la kuonesha nafasi ya elimu, ujuzi na ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya taifa.
Ameeleza kuwa tukio hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wizara, taasisi za elimu ya juu, vyuo vya ufundi na ualimu, taasisi za utafiti, shule, wabunifu, kampuni za teknolojia, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo ili kuonesha mafanikio na kujadili fursa zilizopo katika sekta ya elimu, sayansi na teknolojia.
Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya bunifu na teknolojia kutoka ndani na nje ya nchi, Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU), mashindano ya ujuzi kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi, makongamano ya kitaaluma, warsha na utoaji wa huduma zinazohusu hakimiliki na ulinzi wa bunifu.
Amesema Serikali imeendelea kushuhudia mafanikio kupitia mashindano ya MAKISATU, ambapo bunifu kadhaa tayari zimeingia sokoni na kuwapatia wabunifu wake kipato. Baadhi ya bunifu hizo ni mashine ya kukamua mafuta ya parachichi (Avomero), mabegi ya shule yenye sola za kuzalisha umeme, vifaa vya kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu, teknolojia za usindikaji wa chakula cha mifugo pamoja na mita janja za maji.
Prof. Mkenda amesisitiza kuwa bunifu nyingi hazibaki kwenye maonesho pekee bali zimekuwa biashara halisi zinazochangia ukuaji wa uchumi. Amesema Serikali itaendelea kutoa mazingira rafiki yatakayowawezesha wabunifu kuendeleza teknolojia zao na kuzifikisha kwa watumiaji.
Aidha, amesema kwa sasa Serikali inafuatilia takribani bunifu 70 zilizopo katika hatua tofauti za maendeleo na inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha zinapata nafasi ya kuingia sokoni.
Katika kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini, Prof. Mkenda amesema Wizara imeanzisha Madawati ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika halmashauri mbalimbali kwa lengo la kutambua, kushauri na kuwawezesha wabunifu. Hadi sasa halmashauri 90 zimeanzisha madawati hayo, huku mpango ukiwa ni kuyafikisha katika halmashauri zote nchini.
Ameongeza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, imeweka utaratibu wa kuwawezesha wabunifu kupata mitaji ya kukuza biashara zao. Vilevile, inaendelea kushirikiana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) ili kutafuta masoko mapya, utaalamu na fursa za uwekezaji katika sekta ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazowakabili baadhi ya wabunifu, Prof. Mkenda amesema Serikali itaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha bunifu zinazohitaji uthibitisho wa kitaalamu zinakamilisha taratibu kwa wakati, huku viwango vya ubora na usalama vikizingatiwa, hasa kwa bidhaa zinazohusu afya.
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa taasisi za umma na binafsi, watafiti, wabunifu, wanafunzi pamoja na wananchi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo ili kujionea bunifu za Watanzania na kutumia fursa zitakazosaidia kukuza uchumi na maendeleo ya taifa.