×

Mnyika: Afya ya Lissu Gerezani Siyo Nzuri, Awaomba Watanzania Kumuombea – Video

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amesema hali ya kiafya ya Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, akiwa gerezani siyo nzuri na kuwaomba Watanzania kuendelea kumuombea.

Mnyika ameyasema hayo leo Agosti 3, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo pia amewashukuru Watanzania kwa kuendelea kukisaidia chama hicho katika kipindi hiki cha changamoto.

Amesema Chadema kimepokea jumla ya Shilingi milioni 266 kama sehemu ya mchango unaolenga kufikisha Shilingi milioni 334 kwa ajili ya kuendesha Baraza Kuu la chama hicho linalotarajiwa kufanyika Septemba 15, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mnyika amewashukuru Watanzania kwa kuendelea kukipa chama hicho sapoti kupitia michango yao, akisema msaada huo unakipa nguvu chama kuendelea na majukumu yake.

“Mazingira tunayopitia ni magumu lakini tuna ujasiri wa kuyavuka kwa sababu nyinyi Watanzania mnatuunga mkono. Ahsanteni kwa kutuchangia fedha,” amesema Mnyika.

Ameendelea kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchangia chama hicho, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika kipindi hiki ambacho Chadema kinakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Mnyika amewaomba Watanzania kumuombea Tundu Lissu kutokana na hali yake ya kiafya akiwa gerezani, akieleza kuwa hali hiyo siyo nzuri.

Leave a Comment