×

Polisi Dar Wakamata Watuhumiwa 83, Wabaini Mtandao wa Simu za Wizi

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 83 kwa tuhuma za kuhusika na makosa mbalimbali ya jinai, yakiwemo wizi, ubakaji, mauaji, biashara ya dawa za kulevya na ununuzi wa mali zinazodaiwa kuwa za wizi.

Watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni iliyofanyika mwezi uliopita kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, huku jeshi hilo likiendelea kuimarisha upelelezi ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wengine.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Agosti 4, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema miongoni mwa waliokamatwa ni Mtanko Ebenezer maarufu “China” pamoja na wenzake wawili katika Mtaa wa Amani, Mbezi, Wilaya ya Ubungo.

Kwa mujibu wa Muliro, watuhumiwa hao walikutwa na simu janja 122 zinazodaiwa kuwa za wizi, luninga saba za aina mbalimbali na vifaa vinavyotumika kufuta na kusakinisha upya mifumo endeshi (software) ya simu zilizoibwa kabla ya kuziuza tena.

Katika operesheni nyingine iliyofanyika Matumbi, Wilaya ya Temeke, polisi walikamata kilogramu 75 za bangi aina ya skanka na kuendelea na msako dhidi ya wote wanaohusishwa na usafirishaji, usambazaji na biashara ya dawa hizo.

Operesheni hiyo pia iliwanasa watuhumiwa wanaodaiwa kujihusisha na uvunjaji wa nyumba, wizi pamoja na biashara ya kununua mali zinazodhaniwa kuwa za wizi, zikiwemo simu, luninga, pikipiki, kompyuta mpakato na redio.

Wakati huohuo, Muliro alisema upelelezi wa mashauri yaliyowasilishwa mahakamani kupitia Ofisi ya Mashtaka umeendelea kuzaa matokeo, ambapo baadhi ya watuhumiwa wametiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo mbalimbali.

Miongoni mwa waliotiwa hatiani ni Albert Lisaliko, mkazi wa Kigamboni, ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kulawiti.

Pia, Said Shaban, mkazi wa Mbezi Magufuli, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, huku Madson Mkumbo, mkazi wa Goba, akihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama hiyo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kulawiti.

Aidha, Harun Mustafa, mkazi wa Mbagala Charambe, alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Wilaya ya Temeke baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kulawiti.

Katika hatua nyingine, Muliro alisema Jeshi la Polisi limebaini ongezeko la matukio ya utapeli unaofanywa kwa kisingizio cha biashara za madini, magari, viwanja, mazao na usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari kwenda nje ya nchi.

Alisema jeshi hilo pia limebaini matapeli wanaowadanganya wananchi kuwawezesha kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kwa kutumia hati za nyumba za watu wengine, pamoja na wanaoendesha michezo ya upatu.

Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa wote wanaojihusisha na vitendo hivyo, likisisitiza kuwa linaendelea na uchunguzi na litawachukulia hatua za kisheria wahusika wote watakaobainika.

Leave a Comment