FORT PORTAL, UGANDA: Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi IV wa Ufalme wa Tooro, magharibi mwa Uganda, amezikwa katika Makaburi ya Kifalme ya Karambi, kufuatia kifo chake kilichotokana na saratani mwezi uliopita.
Mfalme Oyo, ambaye alitawazwa Septemba 12, 1995 baada ya kifo cha baba yake, amezikwa Septemba 12, miaka 31 baada ya kutawazwa kwake. Alikuwa ametawala Ufalme wa Tooro tangu akiwa na umri wa miaka mitatu.
Mazishi yake yamefanyika kwa kuzingatia mila na desturi za kifalme za Tooro, huku hafla ya mwisho ya kumzika ikiwa ya faragha na kuhudhuriwa na familia pamoja na marafiki wachache wa karibu.
Wananchi na vyombo vya habari hawakuruhusiwa kushuhudia hatua za mwisho za mazishi, huku kamera zikizuiwa katika eneo la kaburi.

Mapema asubuhi, saa 3:16 kwa saa za eneo hilo, jeneza lililobeba mwili wa Mfalme Oyo, likiwa limefunikwa kwa rangi rasmi za Ufalme wa Tooro, njano na bluu, liliondolewa katika Ikulu ya Karuziika mjini Fort Portal kwa safari yake ya mwisho.
Maelfu ya waombolezaji walikusanyika katika Kanisa Kuu la St. John, kanisa lililojengwa na babu wa Mfalme Oyo, Omukama Rukidi III, na ambako marehemu mfalme alibatizwa.
Mazishi hayo yalihudhuriwa pia na maafisa wa serikali, viongozi waandamizi pamoja na wawakilishi kutoka falme na tawala za machifu wa jadi kutoka Uganda, Kenya, Sudan Kusini, Nigeria na Eswatini.
Kwa mujibu wa mila za Tooro, Omusuna, msimamizi mkuu wa masuala ya kifalme anayehusika na mazishi ya wafalme, aliongoza taratibu za mazishi.
Miongoni mwa desturi zilizotekelezwa ni mfalme mpya kutupa punje tisa za kahawa kaburini, ikiwa ni ishara maalumu katika taratibu za kifalme za Tooro.

Mzozo wa Urithi Wazua Mvutano
Kifo cha Mfalme Oyo kimeibua mvutano ndani ya familia ya kifalme kuhusu mrithi wa kiti cha ufalme.
Mama yake na baadhi ya wanafamilia wamepinga uteuzi wa Edward Rukidi Kijanangoma, mwandishi wa habari wa televisheni, kuwa mrithi wa kiti hicho, wakisisitiza kuwa mtoto wa marehemu mfalme ndiye anayepaswa kurithi nafasi hiyo.
Hata hivyo, Baraza la Wazee wa Tooro limeunga mkono uamuzi wa ukoo wa kifalme wa kumteua Edward Rukidi Kijanangoma kuwa kiongozi ajaye wa Ufalme wa Tooro.
Akizungumza wakati wa ibada ya mazishi, Mkuu wa Ukoo wa Kifalme, Omusuuga Charles Kamurasi, alisema uamuzi huo umefanyika kwa kuzingatia sheria, mila na desturi za Tooro.
“Tunaye mfalme mpya, Edward Rukidi Kijanangoma. Kila hatua tuliyochukua imezingatia sheria na kuongozwa na mila na desturi za Tooro. Tudumishe amani na tutulie,” alisema Kamurasi.
Uganda Yafanya Mazishi ya Kitaifa
Serikali ya Uganda ilimfanyia Mfalme Oyo mazishi ya kitaifa na kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima yake.
Katika taratibu hizo, marehemu mfalme alipewa heshima ya kupigwa mizinga tisa, ishara ya heshima inayotolewa kwa viongozi na watu mashuhuri wa taifa.
Mamia ya waombolezaji walijipanga kando ya barabara kuelekea Makaburi ya Kifalme ya Karambi, wakimsindikiza Mfalme Oyo katika safari yake ya mwisho.
Mazishi hayo yamehitimisha utawala wa Mfalme Oyo, aliyekuwa miongoni mwa wafalme waliotawala kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, baada ya kuvikwa taji akiwa na umri wa miaka mitatu.
Museveni Atoa Heshima
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amemtaja Mfalme Oyo kuwa kiongozi wa kitamaduni aliyekuwa akiwahamasisha wananchi wake kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Katika ujumbe wa rambirambi uliowasilishwa na Naibu Spika wa Bunge, Thomas Tayebwa, Museveni amesema marehemu mfalme alidumisha uhusiano mzuri na Serikali huku akihamasisha maendeleo na kuhifadhi utamaduni.
Aidha, Museveni ametoa wito kwa Waganda kuongeza juhudi katika mapambano dhidi ya saratani na magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Amewataka wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu visababishi vya magonjwa hayo pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kuyazuia.
