VATICAN, Oktoba 18, 2026 — Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo, amesema ataanza kurejea taratibu katika majukumu yake ya kawaida baada ya kufanyiwa upasuaji wa saratani ya mapafu, siku tano zilizopita.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 71 alitoa kauli hiyo Jumapili, alipowasalimia waumini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican, katika tukio lake la kwanza la hadhara tangu kufanyiwa upasuaji huo Jumanne iliyopita.
Akiwa kwenye dirisha la Jumba la Kitume la Vatican, Papa Leo aliwashukuru watu kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa maombi yao na kuahidi kuendelea na majukumu yake kwa utaratibu, akizingatia hali yake ya kiafya.
“Baada ya kuvuka kipindi hiki kigumu, sasa nitaanza kurejea taratibu katika shughuli zangu, kwa msaada wa Mungu na maombi yenu,” alisema Papa Leo.

Papa huyo, ambaye aliruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Gemelli jijini Roma Jumamosi, alionekana akitoka na kufika dirishani bila kusaidiwa, hali iliyowapa matumaini waumini waliojitokeza kumwona.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, madaktari walimfanyia upasuaji wa kuondoa sehemu ya chini ya pafu lake la kulia baada ya kugundulika kuwa na saratani ya mapafu aina ya adenokarsinoma, ambayo ni miongoni mwa aina zinazojulikana zaidi za saratani hiyo.
Madaktari walisema vipimo vya damu na uchunguzi wa kifua vilivyochukuliwa kabla ya kuruhusiwa kutoka hospitalini vilionyesha kuwa hali yake ilikuwa imeruhusu kurejea nyumbani. Pia walieleza kuwa alikuwa na uwezo wa kufanya shughuli za kawaida za kila siku bila msaada.
WAUMINI WAMUOMBEA
Takribani waumini 15,000 walikusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kushuhudia kurejea kwa Papa Leo hadharani, kwa mujibu wa takwimu za Vatican.
Umati huo ulipiga makofi na kushangilia alipojitokeza dirishani. Baadhi ya waumini walionyesha hisia kubwa, huku mtawa mmoja akipiga magoti na kulia kwa furaha.
Kundi la watawa wengine lilionekana likiwa na bango lililoandikwa ujumbe wa kumtakia heri na kumhakikishia kuwa wanaendelea kumwombea.
Katika hotuba yake, Papa Leo pia aliwataka waumini kuepuka ubinafsi na badala yake kumtumikia Mungu kwa moyo wote na bila kusitasita.
RATIBA YAKE BADO HAIJAWEKWA WAZI
Licha ya kuanza kurejea hadharani, Vatican imesitisha shughuli nyingine za Papa Leo hadi angalau Jumatano, Oktoba 21, wakati ambapo anatarajiwa kufanya ibada yake ya kawaida ya hadhara ya kila wiki.
Hata hivyo, Vatican bado haijathibitisha iwapo atashiriki katika tukio hilo.
Papa Leo pia anatarajiwa kutembelea Uruguay, Argentina na Peru kuanzia Novemba 6 hadi 17, 2026, katika ziara ya Amerika Kusini ambayo itahitaji maandalizi na nguvu za kutosha kutokana na ratiba yake kuwa na shughuli nyingi.
Daktari mkuu aliyemfanyia upasuaji, Stefano Margaritora, amesema Papa Leo anaweza kupata nafuu kamili kwa wakati wa ziara hiyo.
Hata hivyo, Katibu wa Jimbo la Vatican, Kardinali Pietro Parolin, ameonyesha tahadhari kuhusu uwezekano wa Papa huyo kuendelea na ratiba yake ya kawaida bila mabadiliko.
Parolin amesema kasi ya shughuli za Papa inaweza kuhitaji kurekebishwa kulingana na hali yake ya afya.
Hali hiyo inaashiria kuwa, licha ya dalili za awali za kuimarika, kurejea kwa Papa Leo katika majukumu yake yote kutategemea maendeleo ya afya yake katika siku na wiki zijazo