×

Aliyekuwa Mbunge wa Iraq Ahmed Al-Alwani Apatikana Ameuawa Beirut, Lebanon

Aliyekuwa mbunge wa Iraq, Ahmed al-Alwani

Aliyekuwa mbunge wa Iraq, Ahmed al-Alwani, amekutwa amefariki dunia ndani ya nyumba moja jijini Beirut, Lebanon, huku mamlaka za nchi hiyo zikianzisha uchunguzi wa mauaji yake.

Mwili wa al-Alwani ulipatikana Jumanne jioni katika nyumba iliyopo eneo la Tariq al-Jdideh, Beirut, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Lebanon na chanzo cha kiusalama kilichozungumza na kituo cha Al Jazeera.

Chanzo hicho hakikubainisha awali mazingira ya kifo chake, lakini chanzo cha mahakama nchini Lebanon kiliiambia shirika la habari la AFP kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha al-Alwani aliuawa kwa kunyongwa.

Katika hatua nyingine, mamlaka zimekamata raia mmoja wa Lebanon anayeshukiwa kuhusika na mauaji hayo, huku polisi wakiendelea kuwatafuta washukiwa wengine wawili raia wa Syria ambao wanadaiwa kutoroka.

Kwa mujibu wa chanzo hicho cha mahakama, washukiwa walikuwa miongoni mwa watu waliomchukua al-Alwani kutoka uwanja wa ndege hadi hotelini alipowasili Beirut wiki iliyopita.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Lebanon, Jaji Ahmed Rami al-Hajj, anaongoza binafsi uchunguzi huo, unaotekelezwa na kitengo cha taarifa za kiusalama cha Jeshi la Usalama wa Ndani nchini humo.

Ofisi ya al-Alwani imetangaza kifo chake na kukitaja kuwa ni mauaji yaliyopangwa, huku ikitaka uchunguzi wa wazi utakaobaini waliohusika kupanga na kutekeleza tukio hilo.

Taarifa ya ofisi hiyo imeeleza kuwa tukio hilo halipaswi kuishia kwenye kutoa salamu za rambirambi na kulaani, bali linahitaji hatua rasmi za kuwawajibisha wote waliohusika.

Al-Alwani alikuwa mwanasiasa wa madhehebu ya Sunni ambaye aliwahi kuiwakilisha mkoa wa Anbar, magharibi mwa Iraq, katika Bunge la nchi hiyo.

Alipata umaarufu mkubwa wakati wa maandamano ya mwaka 2012 na 2013 yaliyokuwa yakipinga serikali ya wakati huo ya Waziri Mkuu Nouri al-Maliki, ambayo waandamanaji waliishutumu kwa ubaguzi wa kisiasa na kuwanyima nafasi Waislamu wa Sunni.

Pia alikuwa mkosoaji mkubwa wa ushawishi wa Iran katika siasa za Iraq na makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na Tehran.

Mnamo Desemba 2013, al-Alwani alikamatwa katika operesheni ya kiusalama iliyofanyika nyumbani kwake mjini Ramadi, ambapo kaka yake na watu wengine kadhaa waliuawa.

Mwaka 2014, alihukumiwa kifo kwa tuhuma za ugaidi, lakini aliachiliwa huru Aprili 2025 chini ya Sheria ya Msamaha wa Jumla ya Iraq baada ya kukaa gerezani kwa zaidi ya miaka 10.

Kwa upande wake, Balozi wa Iraq nchini Lebanon, Mohammed Reda al-Husseini, amesema ubalozi wa nchi hiyo unafuatilia kwa karibu uchunguzi wa mauaji hayo.

Alisema ubalozi unasubiri ripoti ya mwisho kutoka kwa vyombo vya usalama vya Lebanon ili kubaini mazingira kamili ya tukio hilo.

Hadi sasa, mamlaka za Lebanon zinaendelea na uchunguzi huku kukiwa na wito wa kubaini sababu za mauaji hayo na kuwachukulia hatua wote waliohusika.

Leave a Comment