
Na WAANDISHI WETU|RISASI MCHANGANYIKO| MAKALA
BAADA ya wiki iliyopita kuzungumzia U.T.I inavyosumbua wajawazito, leo tutazungumzia tatizo la maambukizi katika njia ya mkojo kijumla, kwa wanawake na wanaume.
Maambukizi katika njia ya mkojo au kama inavyojulikana kwa wengi U.T.I huathiri mfumo wa mkojo ikiwa ni pamoja na Ureter ambayo ni kama bomba linalosafirisha mkojo kutoka kwenye figo, pia kibofu cha mkojo na Urethra.

Ugonjwa huu unaathiri zaidi kibofu cha mkojo na Urethra lakini unaweza pia kuathiri figo. Maambukizi haya yakiathiri sehemu za chini za kibofu cha mkojo kitaalamu huitwa Simple Cystitis au Bladder Infection, na maambukizi hayo yakitokea sehemu za juu za mfumo wa mkojo huitwa Pylonephritis au Kidney Infection.
Tuliona kuwa ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayeitwa Escherichia Coli (E. coli) na tatizo hili husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria ambao makazi yao ya kawaida ni kwenye utumbo mpana na hivyo huwa wanapatikana pia kwenye haja kubwa.
Maambukizi katika njia ya mkojo lazima yawe ni kwenye njia ya mkojo na si pengine popote. Wapo wanawake ambao wamekuwa wakidhani kwamba tatizo la kutokwa na uchafu ukeni ni ugonjwa huu, hilo si sawa kwani huo ni ugonjwa tofauti kabisa na U.T.I.
Tunapozungumzia maambukizi katika njia ya mkojo, inamaanisha ni kutoka eneo la nje ya utupu hadi kwenye kibofu na kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo.
Kama maambukizi yako katika eneo la kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo, kitaalamu huitwa Lower Urinary Tract Infection na yakihusisha eneo la juu ya kibofu jina hubadilika na kuitwa Upper Urinary Tract Infection.
Mara nyingi maambukizi haya kwa wanawake husababishwa na kutojisafisha vizuri sehemu za siri na kuvaa nguo za ndani zilizochafu. Pia huweza kusababishwa na matumizi ya pedi za kike zenye kemikali ya kukata harufu ambazo huua bakteria wa asili wa eneo la sehemu ya siri na kuwapa fursa bakteria wanaosababisha maradhi kuzaliana kwa wingi.
Halikadhalika upungufu wa homoni ya wanawake iitwayo Oestrogen husababisha bakteria wanaosababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuzaliana kirahisi. Matumizi ya baadhi ya dawa kwa muda mrefu, unywaji wa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na kutokunywa maji ya kutosha pia huchangia tatizo hili.
Uwepo wa mawe katika figo na mirija ya figo pia ni mojawapo ya chanzo cha maambukizi haya katika njia ya mkojo. Sababu nyingine inayosababisha U.T.I ni matumizi ya maji machafu wakati wa kujisafisha au kuoga ambayo huweza kuweka bakteria kwa urahisi na kusababisha mwanamke kupata ugonjwa huo.
Uchafu wa vyoo ni sababu nyingine, kwani matumizi ya vyoo ambavyo ni vichafu huweza kusababisha mwanamke kupata U.T.I kwa sababu ndani ya choo kuna bakteria wengi ambao wanaweza kusababisha ugonjwa huo.
U.T.I KWA WATOTO
Matatizo ya maambukizi ya U.T.I licha ya kuwapata zaidi wanawake, huwakumba pia watoto wadogo wa kike kutokana na sababu za kimaumbile ambapo viungo vyao vya uzazi, njia ya mkojo na haja kubwa vipo jirani. Watoto wa kiume ambao hawajatahiriwa nao huweza kupata maambukizi kirahisi ya U.T.I iwapo watajisafisha kwa kutumia maji yasiyo salama ambapo huwa rahisi kwa bakteria kubaki katika ngozi inayoning’inia kama hajatahiriwa.
Pia wanaume watu wazima ambao hawajatahiriwa wanaweza kupata maambuzi ya U.T.I kutokana na sababu tuliyoitaja juu ndiyo maana tohara kwa wanaume husisitizwa.
Maambukizi yanayoshambulia mfumo wa mkojo husababishwa zaidi na bakteria wanaoishi katika mfumo wa haja kubwa kwa kuingia na kujikita katika mfumo wa mkojo.
Bakteria wengine wanaoleta maabukizo katika njia ya mkojo ni wale watokanao na magonjwa ya zinaa kama kisonono, klamidia, Trimonas na fangasi ambapo huwaathiri watu pale wanapojamiiana bila kutumia kinga na watu wenye maradhi hayo.
Ili kuepuka kupata maambukizi katika njia ya mkojo, mara kwa mara ni vyema kutumia kinga na kwa wanawake wanashauriwa kila wanapomaliza kufanya tendo la ndoa wakojoe ili kuondoa bakteria walioingia au waliokaa katika tundu ya mkojo wakisubiri kuingia.
DALILI
Baadhi ya dalili za mtu kuambukizwa bakteria katika njia ya mkojo kubwa ni maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kuwa na rangi ya njano kupindukia na kuwa na harufu kali ijapokuwa siyo kila mwenye dalili hizo ana maambukizi katika njia ya mkojo.
Dalili nyingine za UTI ni maumivu, kutokwa na usaha wakati wa kukojoa, kabla au baada ya kukojoa kukiambatana na maumivu na kuhisi moto wakati mkojo ukitoka.
Baadhi ya wanaume wakati mwingine hutokwa na majimaji katika njia ya mkojo wakati wa kujisaidia haja kubwa, vichomi katika njia ya mkojo, au kuhisi kuwashwa sehemu hiyo, kuumwa kiuno au tumbo, homa kali mara kwa mara na mwili kuwa mchovu, kwa watoto hupoteza hamu ya kula na mwili huonesha kuchoka, husikia maumivu ya chini ya tumbo usawa wa kitovu na huwa hayaishi. Kwa wanaume huhisi hata nguvu za kiume kupungua na wanawake hupoteza hamu ya tendo la ndoa.
TIBA YA U.T.I
Baada ya kuuchambua ugonjwa wa U.T. I tuzungumzie tiba yake. Maambukizi katika njia ya mkojo hutibika kwa dawa mbalimbali za kisasa baada ya kufanyiwa vipimo na kuthibitika kuwa mgonjwa ana maambukizi hayo.
Dawa ambazo anaweza kupewa mgonjwa ni kama vile Ciprofloxacin, Monurol, Furadantin, Sulfam Ethoxazole, Co-trimax, Ampicillin, Gentamicin na kadhalika. Mgonjwa anayesumbuliwa na U.T.I hapaswi kutumia dawa yoyote bila kwanza kupata ushauri wa daktari.
USHAURI
Wanawake wanashauriwa kuepuka kujisafisha sehemu za siri na maji machafu na yasiyo salama, pia kuepeuka kupaka marashi sehemu hizo, ama kutumia pamba zenye kemikali ya kukata harufu kwani hizo huua bakteria wa asili wa sehemu za siri hali ambayo hukaribisha bakteria wa maradhi kuzaliana kwa wingi.
Pia wanashauriwa wanapojisafisha baada ya kujisaidia kuanzia mbele kwenda nyuma, ili kuepusha kuhamisha bakteria walio eneo la haja kubwa na kuingia njia ya mkojo.
Kwa wale walio katika kipindi cha ukomo wa hedhi, wanaweza kushauriana na daktari juu ya kutumia Oestrogen ya ukeni ili kuwasaidia kujikinga na maambukizi ya U.T.I.
Kwa mwanaume maambukizi haya huathiri nguvu za kiume na kujipenyeza hadi katika korodani na huathiri uzalishaji wa mbegu za kiume. Hivyo wanashauriwa kutibu bila kuchelewa ugonjwa huo.
Kwa stori zote kali, Tu-follow
Facebook @Globalpublishers
Twitter @GlobalHabari
Instagram @GlobalPublishers
YouTube @GlobalTVTZ
Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam