×

Man United Ikiendelea Hivi Itatisha

Paul Scholes

Na WAANDISHI WETU| CHAMPIONI IJUMAA| MAKALA

MANCHESTER United, jana ilikuwa uwanjani kukipiga dhidi ya St Etienne katika Europa League, ambapo upande wa pili timu hiyo imetabiriwa kufanya kweli kama itaendelea na mwendo ilionao sasa.

Hayo yamesema na kiungo wa zamani wa United, Paul Scholes alipokuwa akihojiwa juzi, alisifia mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Jose Mourinho huku akiwazungumzia mastaa wa timu hiyo Wayne Rooney na Paul Pogba.

KUHUSU MAENDELEO

Kumekuwa na maendeleo mazuri, miezi miwili mitatu ya kwanza haikuwa mizuri sasa timu inaanza kukaa sawa na mashabiki wanafurahia. Tatizo ni kuwa bado wapo nafasi ya sita, hilo ndilo linatia hofu lakini bila shaka watamaliza katika nafasi nne za juu.

TOP FOUR YAKO

Chelsea, Man City, Man United na ya nne ni kati ya Arsenal au Liverpool.

ULISEMA UNITED YA LOUIS VAN GAAL ILIKUWA INABOA

Sikuwa peke yangu niliyesema hivyo na sikusema Van Gaal ni kocha mbaya lakini aina ya uchezaji wake haikuifaa United. Mourinho amejua mashabiki wanataka nini na amekuwa akijaribu kufanya kile wanachokitaka tangia Oktoba. Wanatengeneza nafasi nyingi, mashabiki wanataka kuona mabao.

Paul Scholes

KUIKOSOA UNITED

Inauma lakini kuna wakati inabidi uzungumze ukweli, sijali kama ni Man United, Chelsea au Arsenal, nitazungumza nitakachokuwa nakiona ni sahihi. Huwa sijali kuhusu kuwakwaza mashabiki au maofisa wa klabu fulani lakini inapokuwa ni kuhusu klabu yako linakuwa jambo gumu.

KUKUTANA NA VAN GAAL

Hapana sijawahi kukutana naye na sidhani kama alikuwa akinihitaji.

MOURINHO NA MAN UNITED

Ana hadhi ya kuwa kocha wa United, muonekano wake na uwepo wake vimekuwa na maana. Kulikuwa na hofu kama ataweza kudumu muda mrefu na ilianza kutokea kukwaruzana na Chris Smalling na Luke Shaw hadharani lakini mambo yametulia sasa.

UNITED KUREJESHA HADI YAKE

Ilikuwa ngumu mwanzoni lakini sasa inawezekana.
MASHABIKI KUKUBALI STAILI YA MOURINHO

Ndiyo wanaikubali taratibu. Mourinho anaenda mwelekeo sahihi japo bado nina hofu kidogo kama wanaweza kucheza dhidi ya timu kubwa kwa sasa, mfano safu ya ulinzi kukabiliana na washambuliaji kama kina Sergio Aguero, Alexis Sanchez na Harry Kane

UWEPO WA ZLATAN IBRAHIMOVIC NA POGBA

Uwepo wao na Henrikh Mkhitaryan umerejesha makali ya vipaji vya juu, waliosajiliwa siku za nyuma hawakuwa vizuri kwa wakati husika mfano waliosajiliwa na Van Gaal hawakupata muda mzuri wa kuzoea mazingira. Pogba, Ibrahimovic na Mkhitaryan wametoka klabu kubwa na tayari walikuwa sawa kwa mapambano.

USHIRIKI KATIKA EUROPA LEAGUE

Kwa kuwa bado nafasi nne za juu hazina uhakika ni vizuri pia wakiongeza nguvu katika Europa ili kama wakichukua wapate nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa.

USHAURI ILI WAFIKE MBALI

Kuna washambuliaji wanatakiwa kuchukuliwa ili wamsaidie Ibrahimovic. Mtu kama (Antoine) Griezmann au Aguero. Wakicheza vizuri kwenye safu ya ulinzi dhidi ya Tottenham Hotspur, City, Chelsea na Arsenal watajua kama wanahitaji mabeki wengine au la. Beki wa kulia, kushoto hawana matatizo, kipa naye siyo tatizo labda Real Madrid wakimchukua (David de Gea).

KUHUSU WAYNE ROONEY

Kuendelea kuanzia benchi kunaweza kusababisha aondoke mapema, kama kipata nafasi anatakiwa kuitumia vizuri kwa kuwa ana ushindani mkali.
Sidhani kama ataendelea kudumu klabuni hapo kwa miaka miwili zaidi kama hali itaendelea kuwa ilivyo sasa .

MARTIAL KUPOTEZA JEZI NAMBA 9

Kuna wachezaji wanajali namba na wengine hawajali, binafsi sina muda na namba. Martial ni kama hakufurahishwa lakini sasa inaonekana ameweka pembeni.