×

SAA 8 USIKU, MWALIMU YAMKUTA NYUMBA NDOGO!

AR ES SALAAM: Ukiona mtu mzima analia, ujue kuna jambo! Saa 8:00 usiku, Jiji la Dar likiwa tulii, idadi kubwa ya watu wakiwa wameuchapa usingizi, mwalimu aliyefahamika kwa jina moja la Lotony wa Kimara amekumbana na mambo mazito baada ya kukutwa ndani ya chumba cha mwanamke aliyedaiwa ni nyumba ndogo ya watu.

MWANZO WA TUKIO

Awali mtu mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alipiga simu kwenye chumba chetu cha habari na kueleza kuwa, ana habari na akataka kukutana laivu na mwandishi ili ampe ishu nzima. Kufuatia ‘tipu’ hiyo, mwandishi wetu alifanya jitihada za kuonana na sosi huyo aliyekuwa akipatikana maeneo ya Kimara jijini Dar, walipokutana simulizi ya habari hiyo ilikuwa hivi:

“Mimi bwana nimekuita nina jambo linaniumiza sana, kwanza nikueleze tu ukweli kwamba nina mke wangu lakini pia nina nyumba ndogo yangu maeneo ya Kimara Golani. Huyo mwanamke nimempangishia nyumba na nimemuwekea kila kitu ndani.

“Nimekuwa naye kwa muda mrefu sana lakni hivi karibuni nimebaini kuna mzee ananimegea penzi langu, jambo hili linaniumiza sana na nimeambiwa huwa anaendaga kwenye kile chumba mimi nikiwa sipo. Halafu sasa si unajua nina mke, kwa hiyo kwenda kumfumania nako naona inaweza kuniletea shida.

Mwandishi: Kama una mkeo, kwa nini ujipe presha na nyumba ndogo ambazo mara nyingi ni pasua kichwa?

Jamaa: Aaah! Si unajua tena, wakati mwingine ni tamaa tu ila usiniulize sana maswali, wewe nishauri tu cha kufanya.

Mwandishi: Achana na hiyo nyumba ndogo, itakuletea matatizo tu. Tulia na mkeo…

Jamaa: Ushauri wako ni mzuri lakini sasa nisikilize nilichopanga kukifanya. Baada ya kugundua kuwa yule mzee ananizunguka, niliongea na yule mwanamke na nikamtishia kuwa, akinificha, nachukua kila kilicho changu na namuacha. Alilia sana, akaniambia hataendelea naye.

Akanitaka tufanye kitu kimoja kwamba ili kumkomesha, siku ambayo yule mzee atakuja, anitonye halafu mimi nikifika pale wala nisifanye vurugu, nimchimbe mkwara tu ili aache tabia hiyo.

Mwandishi: Basi kama ni hivyo, siku ambayo hiyo nyumba ndogo yako itakuambia mwalimu anakwenda, tutonye ili na sisi tuwepo.

Jamaa: Haina shida ila chondechonde, hili suala nataka tulifanye kwa siri, hata polisi hatuna sababu ya kwenda kwa sababu, si unajua yule siyo mke wangu.

Mwandishi: Wala hamna shida.

SIKU ILIYOFUATA

Jumanne iliyopita saa nne usiku, paparazi wetu alipokea simu kutoka kwa sosi huyo akieleza kuwa, siku hiyo ‘mgoni’ wake alipita tu pale kwenye nyumba ya mchepuko wake na kuahidi kwamba kesho kutwa yake (Alhamis) usiku angeenda. “Jamaa bwana inaonekana kanogewa kabisa, leo kapita pale, amemwambia yule mwanamke atakwenda Alhamis, kwa hiyo siku hiyo huenda nikamnasa,” alisema sosi huyo.

ALHAMIS SAA 3 USIKU

Sosi huyo ambaye aliamua kuahirisha kila kitu ili ahakikishe anamnasa mwizi wake alimpigia simu mwandishi wetu saa 3 usiku na kumueleza kuwa, anajisogeza eneo la tukio ili muda wowote akitonywa iwe rahisi kufika hivyo akamtaka naye aanze kujongea. Baada ya mwandishi wetu kupewa taarifa hiyo, alimshitua mwenzake na kuanza safari ya kuelekea Kimara Golani na kufikia kwenye baa moja kisha kumpa taarifa mwenyeji wao.

SAA 7 USIKU…

Wakati waandishi hao wakielekea kukata tamaa, saa 6:15 sosi huyo alituma sms iliyosomeka: ‘Jamaa ndo’ kaingia, njooni.’ Baada ya kuingia meseji hiyo paparazi wetu walisogea hadi kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mwanamke huyo na kumkuta mwenyeji wao ambapo walibuzibuzi pale nje hadi saa 8 walipogonga mlango.

MWALIMU LIVE….

Baada ya mlango kugongwa, ulifunguliwa na moja kwa moja jamaa mwenye mali aliingia na kuwataka waandishi nao waingie ndipo mwalimu huyo alipokutwa akiwa kavua shati, mwanamke naye akiwa na kanga moja (huenda ni kwa sababu ya joto).

“Mimi sitaki tupigizane kelele wala nini, nataka uniambie tu kuwa, huyu ni nani kwako?” jamaa huyo alianza kuchimba mkwara wa kistaarabu huku waandishi wetu wakifanikiwa kupiga picha kadhaa.

Mwalimu huyo baada ya kuona ‘disko limeingiwa na mmasai’ alikuwa mdogo kama piritoni na akawa anatoa maneno ya kuomba msamaha tu huku akieleza kuwa, hakuwa akijua kuwa mwanamke yule ana mtu wake. “Nyie ni wanaume wenzangu jamani, tusaidiane, mimi sikuwa nikijua kuwa ni mtu wako, nisamehe ndugu yangu, nakuahidi namuacha,” alisema mwalimu huyo.

Jamaa: Mimi wala sitaki haya mambo yafike mbali, ila nakuonya, iwe mwanzo na mwisho, hujui nimemgharamikia kiasi gani huyu.

Mwalimu: Nimekuelewa, ila naomba basi uwaambie hawa wasinipige picha, na kazi yangu hii itakuwa aibu kubwa sana.

Jamaa: Kwani wewe ni nani?

Mwalimu: Mwalimu Lotony..

Jamaa: Unafundisha shule gani?

Mwalimu: Sasa mnataka mjue ili iweje, nimeomba msamaha, nisamehe tu.

Jamaa: Tutajie jina la shule unayofundisha ndiyo tukusamehe

Mwalimu: Nafundisha pale…..( anataja jina la shule moja maarufu ya msingi jijini Dar).

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, wawili hao walikubaliana yaishe, onyo likiwa ni kwamba, mwalimu huyo asikanyage tena nyumbani hapo.

IJUMAA ASUBUHI

Kufuatia maelezo ya mzee huyo kuwa ni mwalimu wa shule moja maarufu jijini Dar, mwandishi wetu saa 3:30 asubuhi alitinga kwenye shule hiyo na kukutana na mwalimu mmoja aliyeomba jina lake lisiandikwe gazeti ambaye alisema kuwa hamjui.

“Huyo mwalimu simjui, labda kama kawadanganya ila sura yake siyo ngeni sana.” Gazeti hili bado linaendelea kufanya jitihada za kujua mzee huyo ni mwalimu wa shule gani.

HABARI HII NI FUNDISHO KWA WANAUME

Ukiitafakari kwa makini sana habari hii utabaini kuwa, inatoa fundisho kwa wanaume ambao wamekuwa hawatosheki na wake zao matokeo yake kuwa na nyumba ndogo ambazo zinawaongezea stress za maisha na mzigo wa majukumu.

Iko hivi; wapo baadhi ya wanawake hasa maeneo ya mijini wamekuwa wakijimilikisha wanaume zaidi ya wawili huku mmoja akiwa ndiye aliyegeuzwa ‘boya’ kwa kulipia nyumba na kununua fenicha huku wengine wakiishia kutoa pesa za matumizi.

USHAURI WA BURE

Ni vyema wanaume waliooa wakatulia kwenye ndoa zao na wale ambao hawajaoa, wakatafuta wanawake waliotulia na kuoa ili kuwa na umiliki halali.

STORI: RICHARD BUKOS, UWAZI