ILIPOISHIA:
Nilipogeuka kumwangalia huku pua yangu ikilakiwa na manukato ya bei mbaya, sikuamini kumuona babu akiwa katika suti ya bei mbaya. Nilibakia mdomo wazi. Babu alikuwa amebadilika hakuwa yule mzee wa kijijini mwenye mavazi yasiyo na hadhi.
SASA ENDELEA…
Babu alikuwa amebadilika kwa kiasi kikubwa, alivaa suti nyeupe juu alivaa kofia ya pama rangi ya ugoro na miwani ndogo. Chini alivaa viatu vya ngozi vya rangi ya ugoro iliyofanana na kofia. Mkononi alikuwa na bakora yenye nakshi ya dhahabu.
Kwa jinsi babu alivyobadilika ukikutana naye utajua ni profesa na wala si mganga wa jadi. Nilibakia nimepigwa na bumbuwazi na kujiuliza vitu vya gharama babu kavitoa wapi na alivinunua kwa ajili gani ikiwa kila siku yeye na shamba, shamba na yeye.
“Mjukuu nipo tayari,” babu alinishtua baada ya kuniona nimepigwa bumbuwazi.
“Babu ni wewe?” nilimuuliza mkono mdomoni.
”Heh! Shoga usijirahisi kwa mume wetu bure, kafanyeni kazi iliyowapeleka la sivyo patakuwa hapatoshi,” Rose yalimtoka makavu bila kujua safari ile haikuwa na kingine zaidi ya kwenda kuchuma ndizi kwenye mkungu wao.
“Jamani siwezi kufanya lolote baya, ila leo lazima niseme babu kanifanyia sapraizi, kumbe handsome babu.”
Nilinyanyuka na kuongozana na babu hadi kwenye gari, kwa vile wakeze na watoto wake walikuwa wamesogea karibu na gari tuliwaaga na kuondoka. Ndani ya gari ulinukia uturi wa babu uliokuwa ukipendeza ndani ya pua zangu.
Kwa jinsi alivyokuwa sikuwa na wasiwasi kuingia naye hoteli yoyote tena tukiwa tumeshikana mikono.Tukiwa safarini nilimtupia jicho la wizi babu aliyekuwa ametulia macho yake yakiwa mbele.
“Babu,” nilimwita.
“Mjukuu,” aliitikia huku akinitazama.
“Babu vitu vizuri hivi umevitoa wapi?” nilimtupia swali la kizushi.
“Mjukuu wangu unaniangalia vibaya, nina suti kama hizi ishirini, pea za viatu kumi na nguo za kawaida sanduku tatu.”
“Ha! Sasa hizo nguo zote unazivaa wapi?”
“Historia yangu ni ndefu haitoshi kwa muda huu ipo siku nitakueleza naamini utaandika kitabu jinsi nilivyoingia kwenye uganga, nilikuwa bonge la bishoo.”
“Ha! Sasa uliingiaje kwenye uganga?”
“Ndiyo maana nimekueleza nina historia ndefu na ya ajabu, kwa kifupi kazi yangu si ya kijijini tu, mjini huwa nakuja mara nyingi hivyo siwezi kwenda katika mavazi ya kiganga kila mtu ajue mimi ni nani. Pia nimesha safiri nchi zaidi ya kumi kwa hii kazi yangu.
“Hivi unaweza kusafiri na tunguri mkononi? Lazima ulingane nao kwa kuvaa suti kali inayolingana na wapanda ndege. Pia dawa zangu naweka kwenye Brif case mkononi. Kama hivi nilivyotoka nani atajua mimi mganga? Kama siyo profesa,” kauli ya babu ilinifanya niangue kicheko.
“Mmh! Huko unatumia lugha gani?”
“Kwani wewe unatumia lugha gani unapotoka nje ya nchi?”
“Kiingereza na Kifaransa kidogo.”
“Basi mimi zote hizo nazizungumza kwa ufasaha zaidi.”
“Babu umesoma hadi kidato cha ngapi?”
“Chuo kikuu.”
“Uongo!”
“Ndiyo maana nikakuambia historia yangu ni ndefu bila kurithishwa uganga na babu yangu na shinikizo la majini nami ningekuwa nakula bata kama ninyi.”
“Kwani ilikuwaje?”
“Mjukuu ni historia ndefu ina siku yake.”
“Unajua kuendesha gari?”
“Acha kuendesha, nilikuwa namiliki magari.”
“Nikikuachia utaendesha?”
“Bila shaka.”
Nilisimamisha gari ili nipate uhakika na kauli ya babu kuwa anajua vitu vingi pia aliwahi kumiliki magari. Tulipishana babu alikaa kulia na mimi kushoto, mwanaume alikanyaga mafuta kama hana akili nzuri. Babu alikuwa mahiri wa kuendesha gari kama kazaliwa nalo.
Tuliwahi kuingia mjini tofauti na mwendo wangu, nikamuuliza alipenda tufikie hoteli gani.