×

Niliolewa na mganga kwa tamaa ya cheo kazini-46

ILIPOISHIA:
Katika miaka tisa ambayo niliondoka nyumbani nilishukuru Mungu familia yangu niliikuta ipo katika hali nzuri japokuwa nilikuwa nimempoteza baba yangu kipenzi miaka mitatu iliyokuwa imepita. Nyumba yangu aliyokuwa akiisimamia mama ilikuwa imeisha wakati huo ilikuwa imepangishwa kwa kampuni moja.

Kwa kweli kila nilivyofikiria dhamira yangu na sehemu niliyoangukia muda mwingi nilikuwa nikilia huku nikiwaangalia watoto wangu wadogo wasio na baba tena wenye afya dhaifu.SASA ENDELEA…

Lakini namshukuru mama yangu kipenzi alisimama nami muda wote kunitia moyo na kunieleza nisahau yote kwani ni mapito. Baada ya misukosuko mingi niliamua kuokoka kujikabidhi mikononi mwa Bwana. Namshukuru Mungu niliweza kujengeka kiimani na kusahau yote yaliyopita.

Kutokana na elimu niliyokuwa nayo niliweza kupata kazi katika mradi wa kanisa kama mhasibu mkuu. Japokuwa mshahara haukulingana na elimu yangu lakini namshukuru Mungu maisha yanaenda kama alivyotaka yeye, haikuwa sawa na kukaa bure pia hata umri ulikuwa umekwenda.

Mpaka napata nafasi ya kusimulia mkasa huu ni miaka kumi imepita, wanangu mapacha wakubwa wana miaka kumi na nane, wa kiume yupo kidato cha tatu baada ya kuchelewa kuanza shule, wa kike ameacha shule akiwa kidato cha kwanza baada ya kupata ujauzito, hivi sasa mimi ni bibi nalea mjukuu.

Anayefuata ambaye ni msichana pia ana miaka kumi na sita naye yupo kidato cha tatu kama kaka yake. Wengine wapo darasa la saba na tano, mmoja wa kiume alikataa kuendelea na shule baada ya kujiingiza kwenye mabangi.

Kwa sasa nipo na mwanaume mwingine ambaye nimezaa naye mtoto mmoja kwa hiyo nina watoto saba. Baada ya kufanya kazi ya kuajiriwa kwa muda mfupi na kupata ujauzito nikiwa kazini, nilipopata likizo ya uzazi sikurudi tena kazini niliamua kuacha kazi na kuwa mjasiriamali baada ya kuhudhuria mafunzo kadhaa.

Kwa sasa nafuga kuku wa mayai na nyama na ng’ombe wa maziwa. Maisha yangu namshukuru Mungu yanakwenda vizuri japo nilipata pigo zito la kumpoteza mama yangu kipenzi, iliniuma sana na kuwa vigumu kumtoa akilini, lakini Mungu alinisimamia kunipa ujasiri. Siku zote sitaacha kuwaombea wazazi wangu kwa vile hiyo ni njia yetu sote.
Mkasa huu kila nikiufikiria niliishia kucheka tu, kama kulia nililia sana mpaka nikataka kumkufuru Mungu. Nakumbuka nilifikia wakati wa kutaka kujiua kwa kuiogopa aibu ya wanadamu, msomi kama mimi kuolewa na mganga wa jadi, heri angekuwa kijana lakini kizee kama kile.

Lakini sina budi kumheshimu babu Sionjwi kama mzazi mwenzangu, sikutaka kumlaumu kwa vile niliamini mimi mwenyewe kushindwa kujiamini na kukimbilia nguvu za giza ndizo zilizosababisha safari ya Ulaya kuishia kuwa mke wa mganga.

Kwa vile babu alikuwa na eneo kubwa, mifugo na mashamba vyote viliuzwa na pesa yake tuligawiwa wakeze na kusaidia watoto wake. Kiasi kile kilinisaidia kutanua miradi yangu ili kupunguza ukali wa malezi ya watoto wangu sita.

Bado najiuliza kama mama Sabini asingekuja kijijini maisha yangu yote yangekuwaje? Mwisho napenda kuwaasa wote wanaoamini jitihada hushinda kudra za mwenyezi Mungu. Bidii pekee na baraka za Mungu ndizo zitakazokunyanyua na wala si kitu kingine, si mizizi wala tunguri. Siku zote tumtangulize Mungu mbele kwa kila kitu kwa vile ndiye ajuaye kesho yetu na siyo sisi wanadamu.

Siku zote tamaa mbele mauti nyuma, tuache tamaa ya maisha kwa vile kila mwanadamu ana riziki yake na riziki ya mtu huwa haipotei bali hucheleweshwa. Tumtegemee Mungu kwa kila kitu ili atuongozee maisha yetu.

Asante kwa kupoteza muda wako kunisoma, naomba uchukue mazuri yote na mabaya yawe funzo kwenu.
Mwisho.

Leave a Comment