×

Jeraha Lililojeruhiwa Nchini Ethiopia – 2

ILIPOISHIA:
Waliendelea na utafiti wa mafuta eneo lenye milima Gel’eme Kusini Mashariki ya ziwa Abaya katika mji wa Arba Minch’. Baada ya kukamilisha utafiti wa awali kwa kuweka alama sehemu zote zenye dalili za mafuta walirudi ofisini kwa ajili ya kuandika ripoti na kuiwasilisha makao makuu Caltex nchini Marekani.
SASA ENDELEA…

Siku ya pili helikopta ilitua kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Migie, watoto wengi walisogea kuishangaa na baadhi ya watu wazima. Baada ya kuteremka Mikilas alimuulizia mzee Natnael Behailu, hawakupata shida kuelekezwa kwa vile mzee yule alikuwa maarufu pale.

Hakukuwa na haja ya kupelekwa kwa vile haikuwa sehemu ya kupotea. Walikwenda hadi kwenye eneo lililokuwa na nyumba zaidi ya tano zilizojengwa kwa udongo na paa lake la udongo ‘matembe’ zilizokuwa ndani ya eneo kubwa lenye uzio wa miti ndani kulikokuwa na zizi kubwa la mifugo.

Japo hakukuwa na mlango wa kuingilia kwenye uzio wa nyumba ile lakini kwa ustaarabu walibisha hodi na kukaribishwa na mzee wa makamo aliyekuwa amevaa vazi la lubega.

“Karibuni,” aliwakaribisha kwa lugha ya Kiwolayta ambayo Mikias alikuwa akiifahamu.
“Asante.”

Walipewa viti na kukaa huku mwenyeji wao akimwita mkewe awaletee wageni maziwa.
“Hapana mzee tu..” Mikias alitaka kumkataza lakini Johnson alipinga kauli ile.
“Mikias hapana mwache alete.”

“Refusing shows contempt so we can miss what we want, always slide to succeed,” Johnson alimweleza kwa Kiingereza kumkemea Mikias.
Baada ya muda yaliletwa maziwa kwenye vibuyu vidogo viwili na mwanamke aliyeonekana bado mbichi lakini alikuwa na mtoto wa mwaka mmoja mgongoni. Pia palikuwa na wanawake wengine watano mchanganyiko watu wazima na vijana wote wake wa mzee wa kaya ile.

“Karibuni,” mwenyeji wao alisema huku akijiweka vizuri kwenye kitu.
“Asante,” alijibu Mikias.

“Tuna imani wewe ndiye mzee Natnael Behailu?”
“Ndiyo,” alijibu huku akiwatupia jicho la udadisi.
Bila kupoteza muda Johnson alijitambulisha kwa lugha ya Kiingereza huku Mikias akitafasiri kwa lugha ya Kiwolayta.

“Naitwa Johnson natoka katika shirika la mafuta la Caltex lililopo nchini Marekani ambalo lipo nchini hapa kwa ajili ya uchunguzi wa mafuta eneo la kusini mwa Ethiopia hasa ukanda wa mji wa Arba Minch’ pembeni ya ziwa Ayaba.”

“Ndiyo,” mzee Natnael Behailu alijibu huku akitaka kujua zaidi madhumuni ya ugeni ule japo wazo lake la awali alijua labda amekwenda kununua mifugo.
“Basi mzee nikiwa angani niliweza kumuona binti aliyekuwa akichunga mifugo.”
“Ndiyo,” aliitikia.

“Kwa kweli nilivutiwa na yule binti na kuona ana kitu cha ziada mwilini mwake ambacho kikitumiwa vizuri ataweza kuyabadili maisha ya familia yake.”
“Kitu gani?”

“Nimekuwa nikiwasaidia vijana wa Kiafrika ambao nimewaona wana kitu cha ziada ambacho bila msaada kinaweza kupotea bure, mwili wa binti yako una thamani kubwa sana, kwa vile dunia ya leo kuna miili ya wasichana ambayo ni adimu sana duniani mwanao ni mmoja wa watu hao.”

“Shida yako nini kwa mwanangu?” mzee Natnael Behailu alishtuka kuona mtu mzima kama yule kumtaka mwanaye.
“Mzee wangu shida yangu kumuendeleza kielimu kisha kumpatia kazi ambayo ndani ya miaka mitano ijayo mwanao ataikamata dunia.”
“Kuikamata dunia! Kivipi?”

Ilikuwa ni vigumu kwa mzee Natnael Behailu kumwelewa haraha Johnson, lakini kwa msaada wa Mikias waliweza kumuelewasha mpaka kuwaelewa na kukubaliana kwa mkataba huku akiachiwa pesa nyingi kwa ajili ya kumruhusu mtoto wao kwenda Marekani kimasomo pia kulipwa kiasi cha pesa kila mwaka kama fidia ya kumchukua mtoto wao.

Baada ya makubaliana ya pande mbili ulisainiwa mkataba chini ya mwanasheria wa pande zote.
Kwa vile Johnson alikuwa bado yupo katika kazi ya uchunguzi aliomba ruhusa ya wiki moja kwa lengo la kumpeleka Zinash Marekani. Kabla ya kuondoka Mikias alishtuka pesa iliyotolewa na Johnson kwa msichana mdogo kama Zinash kwa kuona kama zikipotea bure.

Baada ya kusaini mkataba mrefu wa miaka kumi utakaogharimu mamilioni ya fedha, Mikias alimuuliza nini faida ya kupoteza fedha zote kwa msichana dhaifu kama Zinash.
“Swali zuri, Mikias ulifahamu kuwa nchini mwenu kuna madini na mafuta?”
“Sikuwahi japokuwa inawezekana.”

“Basi jicho langu linaona mbali zaidi yako na ndiyo maana leo hii nipo nchini mwenu, kuja kuwatajirisheni kwa kugundua mafuta na gesi iliyo karibu na ziwa Baya. Kwa hiyo ninachokijua kitakuchukua miaka mia kukielewa.”
“Madini mnatumia vifaa maalumu lakini sioni kitu kwa msichana huyu zaidi ya kupoteza fedha.”

“Ndani ya miaka mitano nitafute na uliniulize swali lako ambalo nina imani utakuwa na jibu tayari zaidi ya kunipongeza kwa jicho langu la tai lenye uwezo wa kuona umbali mrefu ulipo mzoga.”

“Kwa hiyo ina maana Zinash umemchukua kama mzoga?”
Kauli ile ilimchekesha Johnson kabla ya kumjibu na kuona jinsi Mikias alivyo na uwezo mdogo wa kuchanganua jambo.

“Mikias mzoga kwa tai una faida au hasara?”
“Faida kwa vile kile ndicho chakula chake.”
“Basi jicho langu kama tai kuuona mzoga ulio mbali, kwangu mimi si mzoga bali madini yanayotembea yenye thamani kubwa.”

“Mmh! Sawa, kama nitakuwa hai hiyo miaka mitano nitakuuliza swali japo sina uhakika kama nitakuwa bado nafanya kazi hii.”
“Nitakuachia mawasiliano yangu ili tuwe tunawasiliana kama nikiondoka.”
“Itakuwa vizuri sana,” Mikias alimwambia Johnson.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika gazeti hili siku ya Jumamosi.

Leave a Comment