
Jumla ya Walimu Wakuu 20,661 wa shule za msingi za Serikali na Sizizo za serikali nchini wamepewa mafunzo kuhusu utekelezaji wa mitaala ya Elimu ya Awali na Msingi iliyoboreshwa mwaka 2023.
Akizungumzia hitimisho la mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imekamilisha kazi ya utoaji wa mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 5 Mei, 2024, na kuhitimishwa tarehe 12 Juni, 2024 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Ameeleza kuwa lengo la Mafunzo lilikuwa ni kuwajengea uelewa wa pamoja wakuu hao kuhusu mabadiliko ya Mtaala wa Elimu ya Awali na Msingi wa Mwaka 2023 ili waweze kusimamia, kutekeleza na kufanya ufuatiliaji kwa ufanisi, huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kugharamia mafunzo hayo.
“Kwanza namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano , Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia na OR-TAMISEMI kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo kwani uwekezaji uliofanyika ni mkubwa ambapo tuna imani walimu wakuu hawa watakwenda sasa kutekeleza mtaala huu ulioboreshwa kama ulivyokusudiwa “alisema Dkt.Komba.

Ameeleza kwamba katika mafunzo hayo walimu hao wamewezeshwa katika mbinu mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji zinazozingatia ujenzi wa umahiri kwa mwanafunzi, Uchopekaji wa Masuala Mtambuka na TEHAMA katika ufundishaji na Ujifunzaji, Mbinu za Ushauri na Unasihi, Upimaji naTathmini, Mbinu za Ufundishaji wa Darasa Kubwa, Salama na Changamshi na uandaaji wa Azimio la Kazi na Andalio la somo kulingana na msisitizo wa Mtaala wa Mwaka 2023 katika kukuza ubunifu, fikra tunduizi, mawasiliano na ushirikiano.
Pia, Dkt. Komba amesema kuwa walimu waliopatiwa mafunzo hayo wamejengewa uwezo wa kutoa msaada kwa mwalimu wa somo pale inapohitajika (mentorship and support) katika maeneo mabalimbali kama vile uandaaji wa somo, azimio la kazi na namna bora ya kutumia mbinu shirikishi zinazozingatia ujenzi wa umahiri;

Aidha, walimu watakuwa na uwezo wa kusimamia na kuendesha vipindi vya Jumuiya za Ujifunzaji katika ngazi ya shule, kujenga uelewa kwa wazazi wa watoto kuhusu mabadiliko ya mtaala ulioboreshwa 2023 kupitia vikao vya kamati za shule na wazazi. Vile vile, kwa kuwa baadhi ya walimu wakuu hao ni watekelezaji/walimu wa masomo husika, wataweza kufundishaji ipasavyo kulingana na mabadiliko ya mtaala katika masomo yao.
Ametaja katika mikoa ya Mara jumla ya walimu 973, Mwanza idadi ya 1115, Shinyanga walimu 710, Simiyu walimu 627, Kagera walimu 1,080, Geita walimu 790, Kigoma walimu 751, Katavi walimu 292, Rukwa walimu 410, Tabora idadi ya 960, Mbeya walimu 882, Njombe walimu 569 na Ruvuma walimu idadi ya 864 wamepatiwa mafunzo hayo.
Wengine ni kutoka katika mikoa ya Songwe idadi ya walimu 530, Mtwara 721, Lindi idadi ya 582, Pwani walimu 802, Dar es salaam walimu 977, Morogoro walimu 1044, Iringa walimu 579, Manyara idadi ya walimu 730, Dodoma walimu idadi ya 896, Singida walimu 689, Arusha walimu 904, Tanga idadi ni 1151 na mkoa wa Kilimanjaro idadi ya walimu waliopata mafunzo ni 1033.