
WAJUMBE na viongozi wa Vicoba (Village Community Bank) wa Kikundi cha Amani cha Mtaa wa Ukombozi, Mbezi-Luis jijini Dar, wamekinukisha na kuzua kimbembe cha aina yake.
Tukio hilo lilijiri Oktoba 13, mwaka huu maeneo hayo baada ya wanachama kuchachamaa na kufunga mtaa kwa lengo la ‘kumchamba’ mwanachama mwenzao aliyetajwa kwa jina moja la Amina.
Amina anadaiwa kukopa fedha kwenye Vicoba na kushindwa kulipa kwa wakati.
MWEKA HAZINA AFUNGUKA
Gazeti la Ijumaa Wikienda lilifika eneo la tukio na kuzungumza na mweka hazina wa kikundi hicho, Chiku Sefu ambaye alidai kikundi hicho kinamdai fedha mjumbe mwenzao Amina kiasi cha shilingi laki tano na thelathini (530,000) ambazo ameshindwa kulipa hadi sasa.
“Kikundi chetu ni cha muda mrefu na huyo mjumbe tulimkopesha shilingi milioni 1.2, lakini amelipa shilingi laki sita na sabini (670,000), iliyobakia imekuwa mbinde mno kulipa.
“Mara nyingi tumekuwa tukimfuata, lakini siku moja alitaka kutumwagia maji ya moto, mtoto wake akamsema, akaacha… tukaondoka na kwenda Serikali ya Mtaa wa Ukombozi ambako tuliwakuta Wajumbe wa Serikali; Hamadi, Ashura na Gumbo ambao walitupokea kisha tukawapa maelezo yetu, wakampa mjumbe mwenzao karatasi ya wito kumfikishia mtuhumiwa.
“Mjumbe alimpelekea barua ya wito, lakini siku ambayo tulipanga kukutana hakuja. Ikabidi tupange siku nyingine kama kikundi, tukamfuata tena ili aweze kulipa au kutupa mali zake ambazo alikuwa ameziweka kama dhamana ikiwemo kitanda, kabati na tenki.
“Lakini cha ajabu hakuja na ilipofika miezi sita, akaja na kusema tumfanyie hesabu ya fedha anayodaiwa huku akiongea kwa kebehi. Tukampigia hesabu, akalipa shilingi laki sita na sabini (670,000) baada ya hapo hakuonekana tena, ndiyo maana tumeamua kumfungia kazi,” alisema mweka hazina.
MJUMBE WA SERIKALI
Akizungumzia kadhia hiyo, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Ukombozi, Hamadi Mbwana alisema alipata malalamiko kutoka kwa wajumbe wa kikundi hicho kuwa wanamdai Amina kiasi cha shilingi milioni 1.2, ila alilipa 670,000 tu ndipo walipomuandikia karatasi ya wito, lakini hakutokea.
“Tulimuandikia karatasi ya wito ili aweze kufika ofisini, lakini hakutokea ndipo baadaye tulimpelekea taarifa tena kuwa ni lazima aje ili aweze kulipa na siku atakayokuja alete na hizo hela anazodaiwa.
“Lakini siku aliyokuja hakuleta hela na wala hakuzungumza kitu chochote. Kuhusu wao kuamua kufanya uamuzi wa kuandamana kwenda kwake hawajanipa taarifa. Ninawaonya wananchi wa mtaa wangu kuwa wawe makini na watu wanaokuwa nao kwenye vikundi hasa vinavyohusiana na hela,” alisema mjumbe huyo
STORI: NEEMA ADRIAN, DAR