×

Penzi Kabla Ya Kifo-12

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Elizabeth alibaki akiwa amesimama kama nguzo ya umeme, hakuamini kile kilichotokea, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, hakutingishika, alibaki vilevile na ghafla machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake.
ENDELEA NAYO…

Usiku, hakulala, alikesha huku mawazo yake yakiwa kwa Edson tu. Kila wakati aliishika simu ile na kuiangalia namba ya Edson, alitamani kumpigia na kuzungumza naye, japokuwa alikuwa ametukanwa lakini hilo wala halikuwa tatizo, vitisho vyote alivyokuwa amepewa kwake havikumuogopesha.

Hakutaka kujiuliza mara mbilimbili, hapohapo akampigia simu Edson huku saa yake ikimwambia kwamba tayari ilikuwa ni saa tano usiku. Simu ile ikaanza kuita, haikupokelewa, iliita na kuita mpaka ikakata.

Hakutaka kuacha, alichokifanya ni kupiga tena, yote hayo, alikuwa akitaka kuzungumza na Edson tu kwani bado moyo wake ulikataa kabisa kumtoa mwanaume huyo. Mara ya pili wala simu haikuita sana, ikapokelewa na sauti ya Edson kusikika:
“Hallo!” iliita.
“Hallo Edson.”

“Wewe Elizabeth! Nilikwambiaje?”
“Nimeshindwa kuvumilia, kama unataka kuniua njoo uniue tu, siwezi kuona nikikukosa, nakupenda sana,” alisema Elizabeth huku akianza kulia.
“Nimekwambia hivi….”

“Ninakupenda Edson, ninahitaji uwe mpenzi wangu!”
“Hivi wewe mwanamke umechanganyikiwa?”
“Ndiyo! Nimechanganyikiwa kwa mapenzi yako, naomba unihurumie Edson….” alisema Elizabeth huku akiendelea kulia.

Huku akiendelea kuishikilia simu, akahisi kulikuwa na mtu alimpokonya mwanaume huyo simu ile, wakati akikaa kusikilizia, mara akasikia sauti ya mwanamke ikianza kuita simuni. Hakutaka kujiuliza, alijua kwamba huyo alikuwa mkewe Edson, hakukata simu, alitaka kusikiliza angesemaje.

“Mbona unatusumbua sana Elizabeth! Hivi haukumuelewa Edson?” aliuliza mke wa Edson kwa sauti iliyosikika kama mtu mwenye wivu mkali.
“Ninajua! Ila ninampenda mumeo!”
“Unasemaje?”

“Ninampenda mumeo! Ni mwanaume wangu wa ndoto, sipendi kulificha hili, mwambie kwamba ninampenda sana,” alisema Elizabeth huku kilio cha kwikwi kikisikika, hakuongea sana, akakata simu hiyo na kuanza kulia kwa sauti kubwa iliyozuiliwa na mto alioulalia kwa staili ya kuufunika uso wake.
*****
Mapenzi ni upofu, ndivyo ilivyokuwa kwa msichana Elizabeth. Alikuwa na jina kubwa, alipendwa na watu wengi, kila alichokifanya, kilionekana kuwa baraka, alifanya biashara nyingi zilizomfanya kuwa bilionea, alijikusanyia kiasi kikubwa cha fedha na kuwa mwanamke aliyekuwa na fedha kuliko wanawake wote barani Afrika, lakini pamoja na kuwa na vitu vyote hivyo, mapenzi yalimtesa, mapenzi yalimliza kila siku.

Mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, hakumpenda kama alivyokuwa akimpenda, aliutesa moyo wake, alishindwa kujizuia. Kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, mapenzi yalimtesa, kuanzia siku hiyo ambapo alimpigia simu na mwisho wa siku kuzungumza na mke wa Edson, hakutaka kuwasiliana naye tena.

Siku ziliendelea kukatika, bado alikuwa na hamu ya kupata mtoto, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, hakuwa na tatizo lolote kiafya, alikuwa mzima kabisa lakini kitu cha ajabu, hakuweza kupata mtoto.

Kila alipowaona wanawake wengine wakiwa na watoto wao, moyo wake ulimuuma mno, alitamani naye kupata mtoto kama wengine, ampende na kumlea kwa mapenzi ya dhati.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake wiki ijayo

Leave a Comment