×

The Angel of darkness – 33

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.

Wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na mapenzi kati ya Arianna na Msuya yanaanza kukolea, jambo linalosababisha Diego awe kwenye wakati mgumu sana kihisia kutokana na wivu uliokuwa ukimsumbua kila kukicha.

Asubuhi moja, kunatokea mvutano mkali kati ya Arianna na Diego, jambo linalosababisha kijana huyo ampige na kumjeruhi vibaya. Anamuomba Arianna amfichie siri lakini Msuya anahisi jambo na kuanza kumbana Arianna kwa maswali.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Hebu nitazame,” alisema Msuya lakini Arianna hakuthubutu kunyanyua uso wake kumtazama. Akajiinamia huku akichezea kucha zake.

“Arianna!” alisema Msuya huku akimuinua Arianna, macho yao yakagongana, wakabaki wametazamana huku Arianna akianza kulengwalengwa na machozi.

Niambie ukweli wa kilichokutokea, nakuomba sana mpenzi wangu,” alisema Msuya huku akiwa amemkazia macho Arianna ambaye alishindwa cha kujibu zaidi ya kuendelea kulia kwa uchungu, akaendelea kumbembeleza na baada ya msichana huyo kutulia aliamua kumueleza ukweli Msuya kwa sababu alikuwa na dukuduku kubwa ndani ya moyo wake ambalo ilikuwa ni lazima apate mtu wa kumfariji.

“Niahidi kama hata nikikueleza ukweli hutakasirika,” alisema Arianna huku akiwa amemkazia macho Msuya ambaye alitingisha kichwa kuonesha kukubaliana na kilichozungumza na Arianna.

Msichana huyo akashusha pumzi ndefu na kuanza kueleza kwamba kulitokea hali ya kutoelewana kati yake na Diego na kwamba ndiye aliyemjeruhi kiasi hicho. Kauli hiyo ilimshtua sana Msuya, akahamaki lakini Arianna akaendelea kumsihi kwamba asimuulize chochote Diego kwa sababu tayari walikuwa wameshafikia muafaka na kumaliza tofauti zao.

“Hata kama ni kaka yako haruhusiwi kunyanyua mkono wake na kukupiga, hilo ni kosa kubwa sana.”
“Msamehe Msuya, unajua alishazoea kupiganapigana tangu tukiwa wadogo sasa naona anashindwa kuachana na hiyo tabia,” Arianna aliendelea kumdanganya Msuya na kumbembeleza atulie, akashusha pumzi ndefu na kujiinamia, ukimya ukatanda kati yao.

“Siku nyingine akirudia sitamvumilia, ni bora nikampangie chumba akae peke yake nitamhudumia kwa kila kitu kuliko kuendelea kuniumizia mke wangu, sitakubali,” alisema Msuya huku akionesha kukasirishwa sana na taarifa hizo.

Arianna akaendelea kumsisitizia kwamba anaomba asiingilie chochote kwa sababu yalikuwa ni mambo yao ya kifamilia na tayari walishayamaliza, jambo ambalo Msuya alilikubali kwa shingo upande.

Akaendelea kumpa pole Arianna na kumtaka siku nyingine akitokewa na tukio kama hilo, atoe taarifa haraka kwake badala ya kukaa na maumivu kwa muda mrefu kama ilivyotokea.

Siku hiyo ilipita, kesho yake asubuhi daktari wa familia alifika nyumbani hapo kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya Arianna ambapo alimpa dawa za kumponyesha haraka majeraha yake na dawa nyingine za kupunguza maumivu kwa lengo la kuhakikisha anapona kabla ya siku ya harusi yao.

Japokuwa Msuya alijitahidi kadiri ya uwezo wake kutomuuliza chochote Diego kuhusu tukio hilo, ule upendo aliokuwa nao awali, ulianza kupungua na akawa anamuona kama kikwazo cha Arianna kuwa na furaha ya kweli.

Kwa upande wake, bila kujua kama Arianna alishamueleza ukweli Msuya, Diego alijifanya kuguswa sana na kilichomtokea msichana huyo, akawa anajitahidi kuwa naye karibu kwa lengo la kutaka amsamehe kutoka ndani ya moyo wake ili mapenzi yao yaendelee kama kawaida.

Siku ziliendelea kuyoyoma kwa kasi, hatimaye Arianna akapona kabisa na zile alama za majeraha zikafutika kabisa mwilini mwake, maandalizi ya ndoa yakazidi kupamba moto.

Kutokana na umaarufu mkubwa aliokuwa nao Msuya, vyombo mbalimbali vya habari, zikiwemo redio na runinga za jijini Arusha na Dar es Salaam, vilianza kuitangaza sana harusi hiyo. Hakukuwa na kadi za kuomba michango ya harusi zilizotolewa kwa sababu kiuchumi, Msuya alikuwa akijimudu vizuri.

“Arifu naskia doni Msuya anavuta jiko?”
“Na mimi nimesikia chalii ‘angu, sijui manzi gani mwenye kismati aliyepata nafasi ya kuolewa na yule mshua,” vijana wawili waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza mashuka ya kimasai kwenye stendi kuu ya mabasi jijini Arusha, walikuwa wakijadiliana kwa Kiswahili chenye lafudhi ya jiji hilo.

Kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele ndivyo gumzo lilivyozidi kuwa kubwa jijini Arusha, kila mtu alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kumuona mwanamke aliyepata bahati ya kupendwa na tajiri huyo aliyekuwa akifahamika sana jijini Arusha na sehemu nyingine za Tanzania na Kenya.

“Arianna!”
“Abee mume wangu mtarajiwa.”
“Nafikiri kila kitu kinaenda vizuri kuhusu maandalizi ya ndoa yetu kama mwenyewe unavyoona. Lakini kabla hatujaingia kwenye ndoa, nilikuwa nahitaji kuzungumza kwa kirefu kidogo na wewe ili hata tukioana, tuwe na uhakika wa maisha yetu,” alisema Msuya jioni moja baada ya kurejea kwenye biashara zake.

Arianna akakaa vizuri kwenye sofa ndani ya sebule ya kisasa ya Msuya, akawa anamtazama kwa shauku kubwa ya kutaka kusikia anataka kumwambia nini. Kuna wakati mapigo ya moyo ya Arianna yalikuwa yakimuenda mbio akihisi huenda Msuya amegundua uhusiano wake na Diego.

“Naona hapa sebuleni hatutakuwa huru kuzungumza kwa kina, twende chumbani kwangu,” alisema Msuya na kumshika mkono Arianna kwa mahaba, akamsaidia kuinuka pale kwenye sofa kisha mkono wake mmoja akauzungusha nyuma ya kiuno cha msichana huyo mrembo.

Taratibu wakaanza kutembea mpaka kwenye ngazi na kuanza kupandisha kuelekea chumbani kwa Msuya.

“Najua nimewahi kukwambia kuhusu suala hili lakini nataka leo nikupe taarifa rasmi,” alisema Msuya na kukaa jirani kabisa na Arianna, juu ya kitanda kikubwa na cha kifahari kilichokuwa ndani ya chumba chake cha kulala. Arianna naye akakaa mkao mzuri kwa lengo la kutaka kusikia atakachoambiwa na Msuya.

“Nimewahi kuoa miaka kadhaa iliyopita na kubahatika kupata watoto wawili, Anselm ambaye hivi sasa ana umri wa miaka tisa na mdogo wake, Mary-Rose ambaye ana umri wa miaka sita sasa.

“Kwa bahati mbaya, mke wangu alifariki dunia miaka minne iliyopita baada ya kupata ajali ya ndege wakati akirejea Tanzania kutokea Ukraine alikokuwa ameenda kwa biashara zetu,” alisema Msuya na alipofikia hapo, alitulia kwa sekunde kadhaa, ukimya ukatawala ndani ya chumba hicho.

“Sasa hao watoto wako wanaishi wapi? Mbona sijawahi hata kuwaona hapa?” Arianna alivunja ukimya, Msuya akainuka na kwenda kufungua begi lake, akatoa picha kubwa iliyokuwa kwenye fremu, akarudi na kukaa kando ya Arianna.

Akamuonesha picha hiyo ambayo Msuya alikuwa amepiga na mkewe pamojana wanaye wawili siku za nyuma.“Wanasoma shule za bweni na kipindi cha likizo huwa wanakuja hapa au wanaenda kwa bibi yao mkoani Kilimanjaro, likizoz hii wameenda kwa bibi yao ndiyo maana hujabahatika kuwaona,” alisema Msuya na kumgeukia Arianna.

“Uko tayari kuishi na wanangu na kuwaonesha mapenzi kama waliyokuwa wakioneshwa na mama yao nitakapokuoa?” Msuya alimuuliza Arianna lakini badala ya kumjibu, msichana huyo alimkumbatia Msuya kimahaba na kumbana kwenye kifua chake, wakawa wanatazamana kimahaba.

“Nimekupenda wewe Msuya, kwa nini nisiwapende na wanao? Nitawatunza na kuwajali pengine kuliko hata mama yao alivyokuwa anafanya,” alisema Arianna, kauli iliyoamsha furaha ya ajabu ndani ya moyo wa Msuya, wakagusanisha ndimi zao na kuanza kuelea kwenye ulimwengu tofauti.

Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia Jumatatu kwenye gazeti la Ijumaa Wikienda.

Leave a Comment