
MAHAKAMA ya Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara imemhukumu Chegera Mayemba (35), mkazi wa Kijiji cha Buchanchari, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukiri kosa la kubaka mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka 10.
Akisoma hukumu katika kesi hiyo ya Jinai Namba 39/2021, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Serengeti, Judith Semkiwa amesema mshitakiwa atatumikia adhabu ya miaka 30 gerezani na kuwa milango ya rufaa iko wazi.
Wakili wa Serikali, Mafuru Moses akisoma hati ya Mashitaka amesema kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Mei 12, mwaka huu huko Buchanchari ambapo alimuumiza mtoto huyo sehemu za siri na kusababisha damu nyingi kuvuja.
Moses ambaye ni Mkuu wa Mashitaka wa Wilaya ya Serengeti ameiambia mahakama kuwa mshitakiwa alimkimbiza mtoto katika Hospitali ya Nyerere DDH kwa ajili ya matibabu akidai kuwa ameangukia jembe,hata hivyo baada ya kufika Polisi kufuatilia PF3 alipobanwa alikiri kumbaka huyo mtoto.
Amesema mtoto huyo alilazwa hapo hospitali baada ya kushonwa sehemu za siri na baada ya kukiri kosa ameomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo.
STORI: Sifael Paul