×

Stanbic Yaunga Mkono Jukwaa la C-Ceos 2026 Kuchochea Utekelezaji wa Dira 2050

Arusha, Tanzania, 24 Septemba 2026 – Benki ya Stanbic Tanzania imetangaza kuunga mkono Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Maafisa Watendaji Wakuu (C-CEOs Forum) 2026, litakalowakutanisha zaidi ya viongozi 700 wa mashirika ya umma, taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo jijini Arusha kuanzia tarehe 27 hadi 30 Septemba 2026.

Jukwaa hilo, linaloandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, litatoa nafasi kwa viongozi hao kujadili namna mashirika ya umma na yale ambayo Serikali ina umiliki wa hisa chache, yanavyoweza kuongeza ufanisi na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Mashirika ya Umma Yenye Ufanisi wa Juu kwa Uchumi Shindani, Shirikishi na Imara katika Kutekeleza Dira 2050”.

Kwa Benki ya Stanbic, udhamini huu ni sehemu ya dhamira yake ya muda mrefu ya kushirikiana na Serikali na mashirika ya umma katika kutafuta suluhisho zinazoboresha utendaji, kuimarisha upatikanaji wa mitaji nafuu na kuleta matokeo chanya yanayoonekana kwa wananchi.

Mashirika ya umma yana nafasi kubwa katika ukuaji wa uchumi kwa kusimamia rasilimali za taifa na kutekeleza miradi katika sekta za miundombinu, nishati, maji, usafirishaji, teknolojia na sekta zingine. Uwezo wake wa kufanya kazi kwa tija na uwajibikaji utakuwa muhimu katika kufikia malengo ya Dira 2050.

Stanbic Bank imesema inalenga kuchangia safari hiyo kwa kutoa ushauri wa kifedha, kuwezesha upatikanaji wa mitaji nafuu, kufadhili miradi ya kimkakati na kutoa huduma bora za kibenki zinazoendana na mahitaji yao. Benki pia itaendelea kutumia uzoefu wake wa ndani ya nchi na mtandao wake mpana uliopo Afrika nzima kuunganisha taasisi za umma na fursa mbalimbali.

“Mashirika ya umma ni kiungo muhimu katika safari ya maendeleo ya Tanzania. Malengo yetu ni kwenda mbali zaidi ya kutoa huduma za kawaida za kibenki kwa taasisi hizi. Dhamira yetu ni kuwa mshirika anayewasaidia taasisi za umma kubadili mipango mizuri kuwa miradi inayotekelezeka na yenye manufaa ya muda mrefu kwa nchi,” alisema Ester Manase, Mkuu wa Wateja Wakubwa na Uwekezaji wa Stanbic Bank Tanzania.

Leave a Comment