The House of Favourite Newspapers

Kisa Wema Kulala Lupango, Mama Wema Hali Mbaya….

Mariam Sepetu mama yake Wema Sepetu

Na WAANDISHI WETU| IJUMAA WIKIENDA| HABARI

DAR ES SALAAM: Hali ni tete! Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutaja majina ya wanaotuhumiwa kujihusisha biashara na matumizi ya madawa ya kulevya wakiwemo mastaa ambapo Ijumaa iliyopita baadhi yao walitii wito na kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar ‘Sentro’ kwa ajili ya mahojiano akiwemo Wema Isaac Sepetu, mama yake mzazi, Mariam Sepetu anaelezwa kuwa katika hali mbaya kutokana na mwanaye huyo kulala lupango.

Wema Sepetu

Chanzo makini kilicho karibu na mama Wema kilieleza kuwa, baada ya Ijumaa, Wema kwenda kuhojiwa Sentro na kulala lupango, hali ya hewa ilibadilika nyumbani kwa mama yake, Sinza-Mori, Dar kwani mzazi huyo presha ilikuwa juu na kusababisha akeshe akilia usiku kucha.

“Yaani siku ya Ijumaa ambayo Wema na wenzake waliotajwa walikwenda kuhojiwa Sentro kisha kulala lupango, ilikuwa ni siku ngumu sana kwa mama Wema kwani alikuwa akilia siku nzima na usiku wake hakulala kabisa hadi kunakucha.

Wema katika pozi

“Alfajiri ya Jumamosi, ilibidi ndugu zake wamfuate na kumchukua, haikujulikana kama walimpeleka hospitali au wapi lakini hali yake ilikuwa mbaya huku akimlilia mwanaye Wema ambaye alilala lupango ,” kilisema chanzo hicho.

WIKIENDA KWA MAMA WEMA

Baada ya habari hizo kutua kwenye meza ya Wikienda, wanahabari wetu walitinga nyumbani kwa mama Wema na kukutana na kijana ambaye alifungua geti kwa nafasi ndogo huku akiwa anaonesha wasiwasi mkubwa na kutetemeka.

Kijana huyo alipoulizwa kama mama Wema alikuwepo alijibu hakuwepo. Alipoulizwa alikokwenda alisema: “Alichukuliwa alfajiri na ndugu zake.” Alipoulizwa hao ndugu zake walimpeleka wapi alijibu: “Sijui’. Alipoulizwa hali yake kiafya ilikuwaje, alifunguka: “Mama yuko kawaida tu.”

Alipoulizwa juu ya Wema kutoka lupango au la, alijibu:

“Kuhusu Wema haishi hapa, yeye anaishi Ununio.”

Alipoona anabanwa zaidi na maswali, alibamiza geti kisha alikaa kimya.

Wema na mama yake.

NYUMBANI KWA WEMA SASA

Wikienda halikuishia hapo  kwani lilifunga safari hadi nyumbani kwa Wema, Ununio ambapo liliwakuta vijana wawili ambao walimtoa nduki huku wakimpopoa mawe mwanahabari wetu wakidai kwamba waandishi ndiyo chanzo cha Wema kuingia kwenye matatizo.

“Ninyi waandishi ndiyo mmesababisha haya yote… ondokeni…” ilisikika sauti ya  kiume inayolazimishwa kuwa nyororo.

MAMA TID NAYE HOI

Marehemu Ngwear (kulia) enzi za uhai wake akiwa na T.I.D

Huko Kinondoni-Sterio, Wikienda lilifika nyumbani kwa akina TID na kukutana na kaka yake aliyemkatalia mwandishi wetu kuingia ndani kufanya mahojiano na mama TID kuhusu msala wa mwanaye.

Kaka huyo ambaye hakutaka jina litajwe gazetini alisema mama yao yu hoi kutokana na presha hivyo hawezi kumruhusu mwandishi kuingia ili kuonana naye kwani alikuwa amelala.

MAMA PETIT MAN KITANDANI

Kwa mujibu wa mwanafamilia mmoja, mama mzazi wa Petit Man ambaye yeye alikamatwa mapema na kuwekwa ndani, naye yu hoi kitandani huko mkoani Iringa kwani baada tu ya kusikia mwanaye yupo lupango, presha ilipanda na kukimbizwa hospitali.

TUJIKUMBUSHE Alhamisi iliyopita Makonda akiwa anazungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ilala-Boma, Dar, alitaja majina ya watuhumiwa wanaojihusisha na madawa ya kulevya na kuwataka siku inayofuata, Ijumaa wafike Sentro kwa ajili ya mahojiano.

Petitman wa kwanza (kushoto) katikati mama Daimond na kulia ni Esma mke wa Petitman

Katika majina hayo walikuwepo mastaa kama Wema Isaac Sepetu, TID, Chid Benz, Nyandu Toz, Babuu wa Kitaa, Recho, Mr Blue na wengine walitajwa Ijumaa ambao ni Vanessa Mdee na Tunda Sebastian waliotakiwa kuripoti leo kwa ajili ya mahojiano.

Baadhi ya waliofika Sentro kama Wema, TID, Babuu wa Kitaa na Nyandu Toz walilala lupango.

Hali hiyo ya kutajwa majina imesababisha Jiji la Dar kwa sasa kuwa la taharuki huku kila kona gumzo likiwa ni hilo na mastaa wengine ambao hawajatajwa wakiwa matumbo joto kuhofia nao kutajwa.

Save

Comments are closed.