×

DC TEMEKE AWAFUNDA WANAVICOBA

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva (watatu kulia), akifuatilia jambo wakati wa maadhimisho ya siku ya Vicoba wilayani humo, kushoto kwake ni  Mratibu wa Vicoba Endelevu Temeke, Johari Mkonde na Bupe Mwakibete (kulia kwake) Katibu Tawala Wilaya ya Temeke

MKUU  wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, amewataka wajasiriamali walio katika mpango wa Vicoba, kutumia vyema huduma za kibenki ili kuondokana na changamoto  ya upotevu wa pesa kwa wanachama wasio waaminifu.

Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Vicoba Wilayani Temeke, yaliyofanyika sambamba na uzinduzi wa jina la  taasisi ya Vicoba endelevu itakayofahamika kama Temeke Pamoja.

“Utumiaji wa taasisi za kibenki ndiyo njia pekee za kuziweka pesa zenu katika mikono salama, na pia inaweza kutumika kupata mikopo, ingawa katika hili ni vyema kuangalia zile zenye riba nafuu,” alisema Lyaniva.

Naye Mratibu wa Taasisi ya Vicoba endelevu Temeke, Johari Mkonde, akielezea maendeleo  ya Vicoba alisema kuwa idadi ya vikundi imeongezeka kutoka 20 vya mwaka jana  hadi kufikia 152.

 

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkonde alimuahidi Mkuu wa wilaya kuwa  atahahakisha idadi ya vikundi kuongezeka maradufu.

“Tunalenga kupata vikundi vingi  zaidi ili tuwe na wajasiriamali zaidi wanaolenga kujiwekea hisa na kukopa lakini kuendeleza miradi yao mbalimbali hasa ukizingatia dhamira tuliyonayo ya kufikia uchumi wa viwanda, ” alisema Mkonde

Nao wanachama wa taasisi hiyo ya Vicoba Endelevu Temeke, wakiwasilisha risala yao kwa Mkuu wa Wilaya walisema wanahitaji  msaada wa kupatiwa eneo kwa ajili  ya kuweka mashine ya kusaga, ambao ni mmoja ya miradi waliyoazimia kuifanya.

“Tunaomba  utusaidie kupata eneo, tupo tayari kuchangia gharama kama kutakuwa  na uhitaji,” alisema Ester Msechu aliyesoma risala hiyo.

Naye Rais wa Taasisi ya Vicoba Endelevu nchini, Devota Likokola, aliwahimiza wanachama hao kujikita zaidi katika uanzishaji wa viwanda vidogo ili kufikia uchumi wa kati

“Hadi sasa Tanzania ina  wanachama wa Vicoba wanaokadiriwa kufikia milioni tano, ikiwa  ni sawa na  asilimia 10 ya Watanzania wote, hivyo kama tukiamua kuanzisha viwanda vidogovidogo, kila mmoja,  maana yake tutakuwa tumekwenda mbele zaidi kwenye suala zima la  kufikia uchumi wa kati,” alifafanua.

HABARI/PICHA: ZAINA MALOGO