Rais Samia Ashuhudia Utiaji Saini Mradi wa Maji kwa Miji 28 Tanzania

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, leo juni 6, 2022, ameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya Mradi wa Maji kwa miji 28, hafla hiyo imefanyika ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Akiongea katika Hotuba yake Rais Samia amesema Serikali ya India imekuwa mshirika mkubwa sana kwa miradi ya maji nchini Tanzania.
Rais Amebainisha kuwa kupitia Benki ya Exim ya India imesaidia mradi wa maji wenye thamani ya Shilingi Bilioni 617 ambao umepeleka maji kutoka Ziwa Victoria hadi katika maeneo ya Tabora Igunga na Nzega ambapo jumla ya vijiji 102 vimenufaika na mradi huo ambao unaenda hadi mkoani Shinyanga.

Rais Samia amesema Serikali ya India imeipatia Tanzania mkopo wa dola milioni 500 ambapo kwa kiasi kikubwa pesa hiyo itafanya kazi Tanzania Bara huku kiasi kidogo kikielekezwa Visiwani Zanzibar kufanya kazi hiyohiyo ya maji.

Kwa kipekee Rais Samia ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya India kwa ushirikiano inaoutoa kwa nchi ya Tanzania huku akibainisha kuwa nchi hiyo imekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania si tu kwenye Nyanja ya maji lakini pia kwenye Nyanja nyingine kama ya biashara na uwekezaji.
Kwa upande mwingine Rais Samia ameipongeza Wizara ya Maji chini ya Waziri Jumaa Aweso kwa kazi nzuri inayoifanya huku akiwahakikishia wananchi kuwa mradi huo mkubwa wa maji hautaacha mji hata mmoja kati ya miji yote 28 iliyoainishwa katika mradi huo.