The House of Favourite Newspapers

Vodacom Tanzania Foundation Na JKCI Washirikiana Kupanua Huduma Za Moyo Kwa Watoto

0

Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc Philip Besiimire akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Heart Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naizihijwa Majani baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto hapa nchini kwa kuchangia asilimia 30 za gharama ya matibabu ambapo asilimia 70 zikiwa zimelipwa na serikali.

Dar es Salaam, 29 Septemba 2025 – Vodacom Tanzania kupitia asasi yake leo imesaini Makubaliano (MoU) na Heart Team Africa Foundation, asasi maalumu iliyoko chini ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ikiwa ni hatua kubwa katika kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto hapa nchini. Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo imefanyika sambamba na Siku ya Moyo Duniani 2025, chini ya kaulimbiu “Don’t Miss a Beat”, ikihimiza kuchukua hatua mapema na kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa afya ya moyo.
Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili, inakadiriwa kuwa watoto wawili kati ya kila watoto 100 huzaliwa na ugonjwa wa moyo(Congenital Heart Disease – CHD), na asilimia tatu ya watoto wenye umri wa miaka 5–15 huathiriwa na Ugonjwa wa Moyo wa Rheumatic (RHD) hali inayoweza kuzuilika endapo maambukizi ya koo yatatibiwa mapema.
Kila mwaka zaidi ya watoto 4,000 wanahitaji upasuaji, lakini bado huduma hazipatikani kwa urahisi. Ingawa Serikali inagharamia asilimia 70 ya matibabu, asilimia 30 iliyobaki bado ni mzigo mkubwa kwa familia nyingi. Kwa sasa JKCI ina zaidi ya watoto 350 wanaosubiri upasuaji.
Akizungumzia ukubwa wa tatizo, Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI alisema, “Kila takwimu inawakilisha mtoto mwenye ndoto na mzazi mwenye matumaini. Ushirikiano huu utatusaidia kupunguza pengo kati ya uhitaji na upatikanaji wa huduma, ili kuhakikisha watoto wengi zaidi wanaishi maisha yenye afya njema.”
Naye Dkt. Naizihijwa Majani, Mkurugenzi Mtendaji wa Heart Team Africa Foundation na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto aliongeza, “kila siku tunaona jinsi gharama za matibabu zinavyoweza kuwa kizuizi kati ya mtoto na mustakabali wake. Ushirikiano huu wa Vodacom na JKCI sio tu msaada wa kifedha, bali ni njia ya kuokoa maisha. Kwa pamoja, tunajenga Tanzania ambayo hakuna mzazi anayelazimika kuchagua kati ya umasikini na mapigo ya moyo ya mtoto wake.”
Mapema mwaka huu, Vodacom Tanzania Foundation ilizindua Amini Initiative huko Visiwani Zanzibar, ikiahidi kudhamini watoto 150 kwa kugharamia asilimia 30 ya gharama zinazobaki za matibabu. Mpaka sasa watoto 38, wenye umri kati ya miezi miwili na miaka 14, wamefanyiwa upasuaji kwa mafanikio.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Philip Besiimire, Afisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, alisema, “huu ni wakati wa kuchukua hatua na ndiyo maana tuko hapa. Makubaliano haya ni ishara thabiti ya kugeuza imani kuwa vitendo kupitia Mpango wa Amini. Tukishirikiana na JKCl, tunafungua kesho ambayo hakuna mtoto atakayepoteza maisha kwa kukosa huduma za kitabibu zinazoweza kuokoa maisha. Badala yake, kila mtoto atapewa nafasi ya kupona, kuwa na matumaini, na kustawi.
Vodacom Tanzania Foundation, JKCI na Heart Team Africa Foundation wanatoa mwito kwa washirika, wafadhili na wadau mbalimbali kuungana nao katika jukumu hili la kuokoa maisha:
“Huu ni wito wa kitaifa. Tunawaalika serikali, kampuni na watu binafsi kusimama nasi, ili mtoto wa Kitanzania asibaki akisubiri upasuaji unaookoa maisha.
Leave A Reply