The House of Favourite Newspapers
gunners X

AMSONS Yasaini Makubaliano ya Mradi wa Umeme Jua wa Dola Mil. 600 Zambia

0

Kampuni ya Kitanzania ya Amsons Group, mojawapo ya kampuni kubwa za nishati barani Afrika, imetangaza ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya Exergy Africa Limited ya Zambia kujenga na kupanua miradi ya uzalishaji na miundombinu ya nishati nchini humo.

Mradi huo utahusisha megawati 1,000 za umeme wa jua na megawati 300 za umeme wa makaa ya mawe, kwa uwekezaji wa jumla wa Dola za Marekani milioni 900 ambapo Dola milioni 600 ni kwa ajili ya umeme jua na 300 kwa ajili ya makaa ya mawe.

Makubaliano hayo ambayo ni sehemu ya mkakati wa Amsons wa kupanua biashara katika sekta ya nishati, yanajumuisha uwekezaji katika kituo kikubwa cha umeme wa jua chenye uwezo wa Gigawati 1 (GW) kupitia Africa Power Generation, muunganiko wa wawekezaji wa nishati jadidifu uliosajiliwa Zambia.

Hafla ya kutiwa saini ilifanyika Ikulu ya Zambia hivi karibuni, na kuongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Edha Nahdi, chini ya uwepo wa Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema. Rais Hichilema alisisitiza umuhimu wa uwekezaji huo katika kuongeza usalama na mseto wa nishati nchini humo.

“Uwekezaji huu wa gigawati 1 ni mabadiliko ya mchezo. Unakabili moja kwa moja uhaba wa nishati nchini kwa kutoa umeme wa uhakika, safi na usiotegemea mabwawa,” alisema Rais Hichilema.

Rais Hichilema aliipongeza Amsons Group akiitaja kama kampuni inayoheshimika barani Afrika, na kwamba mradi wao wa nishati ya jua utaiwezesha Zambia kutimiza, na huenda kuzidi, lengo lake la kuongeza megawati 1,000 za nishati ya jua kwenye gridi ya taifa, hatua ambayo itahakikisha kukoma kwa mgawo wa umeme na kuweka mazingira thabiti ya ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Nahdi alisema Amsons Group na wadau wake wanajivunia kushirikiana na Zambia katika mradi ambao unachochea mabadiliko ya kimkakati kwenye sekta ya nishati.

“Mradi huu hauhusu tu kuzalisha umeme, bali kujenga ajira endelevu, kuongeza uwezo wa ndani na kujenga mifumo imara ya nishati itakayohudumia makazi, shule na viwanda kwa miongo ijayo,” alisema Nahdi.

Uwekezaji wa Dola milioni 600 katika kituo cha umeme wa jua chenye uwezo wa 1 GW unatajwa kuwa moja ya miradi mikubwa zaidi ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) katika sekta ya nishati Zambia na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mradi huo unatabiriwa kupunguza utegemezi mkubwa wa Zambia kwa umeme wa maji, hali iliyosababisha upungufu wa umeme kutokana na ukame unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi wa Exergy Africa Limited, Monica Musonda, alisema ushirikiano huo unaonesha kuongezeka kwa kasi kwa juhudi za Kiafrika kuunganisha sekta ya nishati na kutatua pengo la miundombinu kwa kutumia ushirikiano wa biashara zenye mizizi barani.

Naye Waziri wa Nishati nchini Zambia, Makozo Chikote, alisema serikali inaendelea kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi kama ishara ya mkakati imara wa nishati unaohusisha ushindani na ubunifu baina ya sekta binafsi na ya umma.

Makubaliano haya yanakuja siku chache baada ya Amsons Group kukamilisha ununuzi wa kampuni ya Bamburi Cement nchini Kenya na kuongeza umiliki wake kwenye East African Portland Cement (EAPC), hatua inayoonesha dhamira ya kampuni kuwekeza kwenye mnyororo mpana wa miundombinu na viwanda barani Afrika.

Amsons Group inafanya shughuli zake katika nchi tano za Afrika- Tanzania, Kenya, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Zambia ambako imewezesha kupatikana zaidi ya ajira 10,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Leave A Reply