TRA na Sudan Kusini Kuanzisha Ushirikiano Wa Pamoja Kudhibiti Mianya ya Ukwepaji Kodi

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Sudan Kusini (SSRA) zinatarajia kuanzisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ya kodi ikiwemo kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi baina ya mamlaka hizo mbili.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha pamoja baina ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda na Kamishna Mkuu wa SSRA Bw. William Anyuon Koul kilichofanyika Januari 22.2026 katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mwenda amesema miongoni mwa maendeo watakayoshirikiana ni kudhibiti ukwepaji kodi kwa kuweka udhibiti wa mizigo inayosafirishwa kupitia Bandari za Tanga na Dar es Salaam kuelekea Sudan Kusini.
Amesema Sudan Kusini inalenga kutumia kikamilifu Bandari za Dar es Salaam na Tanga kupitisha mizigo yao na wameomba kutengewa eneo maalum la forodha kwaajili ya kusimamia mizigo yao na kuhakikisha inafika kwa wakati na kwa usalama.
Amesema ili kufanikisha hilo wamekubaliana kujenga mfumo wa pamoja baina ya SSRA na TRA ili kuwezesha mifumo yao kusomana kwa lengo la kudhibiti mapato na kuziba mianya ya Rushwa jambo ambalo litakuwa na manufaa kwa nchi zote mbili.
Kuhusu kujenga uwezo kwa watumishi Kamishna Mkuu Mwenda amesema wamekubaliana kushirikiana kuwajengea uwezo watumishi wao ambao watabadilishana uzoefu na wa utendaji kazi na watumishi wa TRA.
“Tutaingia makubaliano hivi karibuni kalba ya mwisho wa mwezi wa pili na SSRA kwaajili ya kushirikiana kujenga uwezo kwa watumishi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika pande zote mbili na kupata uzoefu wa utendaji kazi kutoka mamlaka zote mbili” amesema Mwenda.

