Klabu ya DTB Imefanikiwa Kupanda Daraja, Kucheza Ligi Kuu Msimu Ujao

KLABU ya DTB inayomilikiwa na Taasisi ya Kifedha ya Benki ya Diamond Trust imefanikiwa kupanda daraja kutoka Ligi daraja la kwanza hadi Ligi Kuu ya NBC na sasa inatarajiwa kushiriki Ligi kuu msimu ujao.
DTB imefanikiwa kupanda daraja baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba katika bao likifungwa na Joel Madondo kwenye mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.
Kwa sasa klabu ya DTB imebakiwa na michezo miwili ambayo ni ya kukamilisha ratiba, michezo hiyo ni dhidi ya Mashujaa ya Kigoma ambao unatarajiwa kuchezwa Mei 14 na dhidi ya Kitayosce ya Tabora unaotarajiwa kuchezwa Mei 21.

Hadi sasa DTB ina jumla ya alama 65 baada ya kucheza michezo 28 ikifanikiwa kushinda michezo 20 kusuluhu 5 na kufungwa 3.