The House of Favourite Newspapers

MKATABA – 1

0

MKATABA – 1

KICHAA cha moyo kilimpanda ghafla Suma. Ni mara ya tatu sasa anamwita msichana huyo lakini haoneshi dalili ya kumwitikia. Suma akazidi kuchanganyikiwa.

Kwa nini haitikii? Akajiuliza mwenyewe kichwani mwake bila kupata jibu.

Ni kama msichana huyo alikuwa hamfahamu kabisa au alimuona kama mhuni tu! Aligeuka mara moja tu na kumwangalia kisha akaonesha kama hamfahamu kabisa.

“Huyu mwanamke amechanganyikiwa nini?” akawaza Suma kichwani mwake.

Msichana aliyekuwa mbele yake akitembea kwa miguu alimfahamu vizuri sana. Alikuwa ni mke wake mpenzi, Zainabu. Siyo mke wa kuokota barabarani, alikuwa mkewe wa ndoa!

Pamoja na kuwa na uhakika na jambo hilo, Zainabu hakuitika kabisa. Alikuwa kimya akiendelea na hamsini zake. Suma akapata wazo jipya ambalo aliamini lingeweza kumsaidia; aliamua kuegesha gari kisha akashuka na kuanza kumkimbilia Zainabu.

Alikuwa na maswali mengi sana kichwani mwake; iweje mkewe aondoke nyumbani wakiwa hawana ugomvi wowote? Nini kimetokea? Hayo ndiyo yaliyoutesa ubongo wake na kupoteza furaha kabisa. Ni muda mfupi tu alimuacha mkewe nyumbani, lakini aliporudi hakumkuta na alipompigia simu akagundua kwamba aliiacha nyumbani kwa sababu simu yenyewe iliitia chumbani kwao.

Kitu alichokiamua ilikuwa ni kumfuatilia nyumbani kwao ili kujua kama alikwenda huko, akiwa njiani tena mita chache sana kutoka nyumbani kwake anakutana  na mke wake lakini akimwita haitiki.

“Zainabu una nini? Hebu subiri basi,” alisema Suma, sasa akimsogelea karibu zaidi mke wake na kumtaka asimame.

Akasimama.

“We’ kaka mbona king’ang’anizi hivyo?” Zainabu akamwuliza.

“Enheeee?!!!” Suma akaonesha mshangao.

Alikuwa na haki ya kushangazwa na kilichokuwa kikifanyika mbele yake, maana alikuwa na uhakika kuwa alikuwa akizungumza na mkewe, Zainabu.

“Mimi ni kaka?”

“Kwani ni nani?”

“Zainabu una kichaa?”

“Kichaa? Halafu nani amekuambia jina langu?” akauliza Zainabu.

“Mh!” akaguna Suma akizidi kuchanganyikiwa kabisa.

Alishindwa kuelewa kilichotokea, hakuelewa mkewe alipatwa na jambo gani.  Alifikiria kwa muda, hakupata jibu. Akaamua kuchukua uamuzi…

“Ngoja niondoke zangu,” akajisemea moyoni mwake.

“Nashukuru sana Zainabu, asante sana,” akasema Suma kisha akarudi kwenye gari lake.

Aliendesha gari hadi nyumbani kwake Mbezi Beach. Hapakuwa mbali sana na eneo lile. Aliegesha gari na kuingia moja kwa moja ndani. Aliishia sebuleni kwake. Akaketi kwenye sofa kubwa kisha akatulia akitafakari kitu cha kufanya.

“Zainabu ananijibu hivyo mimi? Sawa bwana, lakini najua atakuja tu hapa nyumbani. Nitamalizana naye hapa hapa,” Suma akawaza kichwani mwake.

Katika tafakuri hiyo, akajikuta ghafla amepatwa na usingizi mzito…macho yalianza kulegea, akijihisi kama amekunywa pombe, uzito ulipozidi machoni, hakuwa na ujanja, akayafumba!

Hakujua ilivyokuwa lakini alijikuta akiingia katikati ya usingizi mzito sana. Usingizi ambao baadaye ulizaa ndoto!

***

Uso wake ulikuwa umefura kwa hasira. Alikuwa akimsubiri kwa hamu sana mkewe ili amweleze alipokuwa na pia amwambie ni kwa nini alimkana pale barabarani alipokutana naye wakati akimtafuta. Suma akiwa sebuleni hana hili wala lile, mlango mkubwa wa sebuleni ukafunguka.

Zainabu akaingia akitabasamu. Alikuwa na uhakika wa asilimia zote kuwa aliyekuwa akiingia pale sebuleni alikuwa mkewe. Hakuwa na wasiwasi wowote na hilo.

Wakati akiwa na uhakika huo, pia alikuwa na uhakika kuwa Zainabu aliyekuwa akiingia pale sebuleni ndiyo yuleyule aliyekutana naye njiani na akamkana. Alikuwa amevaa nguo zilezile, akinukia manukato yaleyale, kwa hiyo alikuwa na uhakika wa moja kwa moja kuwa aliyekuwa mbele yake alikuwa ni Zainabu mke wake kipenzi!

“Umenifanyia nini Zainabu?” Suma akauliza kwa ukali.

“Tulia Suma, kuna kitu ambacho hukifahamu.”

“Kitu gani?”

“Mimi kuanzia leo siyo mkeo tena.”

“Unasemaje wewe?” Suma akauliza kwa ukali.

“Huna haja ya kuwa mkali maana na mimi nikikasirika utaumia wewe, elewa kwamba tangu sasa mimi si mke wako. Jingine ujue kuwa mimi siyo Zainabu. Kubwa na la msingi zaidi, unatakiwa kufahamu kwamba mkataba wangu na wewe umekwisha!”

“Mkataba?”

“Ndiyo…tulikuwa na mkataba lakini wa siri sana. Umeufanya kati yako na mimi. Umefika mwisho.”

“Sikuelewi Zainabu.”

“Utanielewa tu Suma, inanipasa sasa niende. Nahitaji kukuachia maisha yako.”

Alihisi kichwa kuvurugika lakini pia hakuwa na uwezo wa kukiweka sawa. Kama ni kufikiri, alikuwa ameshafikiria kwa kiwango cha mwisho. Ubongo wake ulikuwa umegonga mwamba.

“Zainabu,” akaita Suma.

“Mara ngapi nikuambie mimi siyo Zainabu ili unielewe?”

“Mpaka muda huu sijaelewa chochote kutoka kinywani mwako.”

“Utaelewa tu.”

“Sitaki unichanganye zaidi, niambie ni kwa nini unafanya haya yote?”

“Nilichotaka kwako nimeshakipata ndiyo maana nimekuambia ni vyema nikuache na maisha yako.”

“Zainabu una nini?”

“Nimeshakuambia mimi siyo Zainabu, mbona huelewi wewe?” akasema Zainabu kwa hasira sana.

Ghafla uso wa Zainabu ukafura kwa hasira, mara akaanza kubadilika na kuwa na macho mekundu sana. Suma akatetemeka kwa hofu. Lilikuwa tukio la ghafla sana kutokea kwake.

Akapiga kelele…

***

“Mamaaaaa nakufaaaaaaa….” Suma alipiga kelele akiwa amekaa kwenye kochi pale sebuleni.

Alishtuka sana, jasho jingi likaanza kumchuruzika mwilini mwake. Hapo sasa akawa na uhakika wa asilimia zote kuwa alikuwa anaota, tena ndoto yenyewe ilikuwa ya kutisha sana.

“Ni ndoto! Mungu wangu…” akajisemea peke yake moyoni mwake.

“Hauoti Suma,” akasikia sauti ya mkewe ikimjibu kwa utaratibu kabisa.

“Nani wewe?” akauliza kwa sauti ya juu akiwa amechanganyikiwa kabisa.

Alikuwa na uhakika mle ndani alikuwa peke yake. Hata alipoingia hakuna mwingine aliyeingia nyuma yake. Sauti ilikuwa ya Zainabu na nyumba ile waliishi wawili tu. Yeye na mkewe Zainabu.

“Mimi…”

“Zainabu?”

“Nimeshakuambia mimi siyo Zainabu ila niliyekuwa Zainabu.”

“Uko wapi?”

“Kwani wewe unasikia sauti inatokea wapi?”

Kwa kiasi fulani, Suma alianza kujiona mjinga maana ni kweli alisikia sauti ikitokea ndani ya chumba chao cha kulala. Suma akasimama haraka ili aende kule chumbani akaulizane vizuri na mkewe.

“Nooooo!” sauti ya Zainabu ikasikika ikitamka.

“Una nini wewe?”

“Suma?” sasa sauti ya Zainabu ilisikika kwa woga sana.

“Vipi mke wangu?”

“Kwa nini unanitesa hivi?”

“Nimekutesa mimi?”

“Ndiyo, umenitesa sana, umeuumiza moyo wangu. Kwa nini unanifanyia haya yote?” Zainabu akasema akiwa mle chumbani.

Suma akachanganyikiwa…

“Kwa nini hutaki niingie chumbani?”

“Hutaweza kuingia humu, umeshaharibu!”

“Nimeharibu?”

“Ndiyo umeshaharibu.”

“Kivipi?” Suma akasema akijaribu kusukuma mlango ili aingie ndani.

“Mamaaaaa!” Suma akapiga kelele za woga.

Kitu alichokutana nacho kilimtisha sana. Chumba kizima kilikuwa kinawaka moto, lakini hakiteketei. Mbaya zaidi hakumuona Zainabu wake.

“Nilikuambia humu hakukufai na hutaweza kuingia.”

“Zainabu uko wapi?”

“Nipo humu ndani?”

“Huo moto umetokea wapi?”

“Umesababisha wewe. Lakini nakuuliza kwa mara nyingine tena, kwa nini unanitesa kiasi hiki mpenzi wangu?  Kwa nini unanyima amani? Ndiyo maana nimeamua kuondoka.”

“Hivi naota au nipo macho?” Suma akawaza kichwani mwake akizidi kutetemeka kwa hofu.

Cha kushangaza sasa, Zainabu alimjibu mle chumbani…

“Huoti Suma, kila kitu ni cha kweli…” sauti hiyo ilisikika huku moto ukianza kutoka chumbani na kuelekea kwenye korido alipokuwa amesimama.

Hakuwa na muda wa kusubiri tena, Suma aliondoka mbio hadi nje alipoingia kwenye gari lake haraka sana na kwenda nyumbani kwa Ustaadhi Alii. Aliegesha gari nje na kushuka haraka kisha kuingia ndani ya geti bila hodi.

“Samahani nimemkuta Ustaadhi?” akauliza mabinti waliokuwa wamekaa pale nje.

“Ndiyo yupo. Mbona hivyo kaka?”

“Hapana, ninachoomba kwa sasa ni mnisaidie kumuita tu. Hilo tu!”

Haraka mmoja wao akaingia ndani, hakukawia sana, tayari Ustaadhi Alii alikuwa ameshatoka nje, naye alikuwa anatweta.

“Vipi Suma?”

“Mtihani Ustaadhi.”

“Nini?”

“Twende nyumbani.”

Ustaadhi hakukaidi, wakatoka pamoja hadi nje ambako waliingia kwenye gari na safari ya kwenda nyumbani kwa Suma ikaanza. Hapakuwa mbali sana na nyumbani kwa Ustaadhi Alii.

 

Endelea kufuatilia simulizi hii hapa kila siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa. Unaweza kunifuata kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii, Facebook: simulizi za joseph shaluwa, Instagram: @joeshaluwa, like kurasa hizo kwa burudani zaidi…

 

ITAENDELEA JUMATANO…

Leave A Reply