MKATABA – 2
ILIPOISHIA JUMATATU…
Haraka mmoja wao akaingia ndani, hakukawia sana, tayari Ustaadhi Alii alikuwa ameshatoka nje, naye alikuwa anatweta.
“Vipi Suma?”
“Mtihani Ustaadhi.”
“Nini?”
“Twende nyumbani.”
Ustaadhi hakukaidi, wakatoka pamoja hadi nje ambako waliingia kwenye gari na safari ya kwenda nyumbani kwa Suma ikaanza. Hapakuwa mbali sana na nyumbani kwa Ustaadhi Alii.
SASA ENDELEA…
USTAADHI hakukaidi, wakatoka pamoja hadi nje ambako waliingia kwenye gari na safari ya kwenda nyumbani kwa Suma ikaanza. Hapakuwa mbali sana na nyumbani kwa Ustaadhi Alii.
Isingekuwa rahisi hata kidogo kwa Ustaadhi Alii kuvumilia hali aliyomuona nayo Suma. Akajikuta akishawishika kumuuliza mapema kabla hawajafika nyumbani.
“Kwani kuna nini nyumbani?”
“Acha tu.”
“Vipi?”
“Balaa tupu.”
“Nataka kujua Suma.”
“Twende utakwenda jionea mwenyewe.”
“Ni vyema uniambie ili nione kama kuna ulazima wa kuongeza nguvu.”
“Mauzauza nyumbani kwangu. Mke wangu amebadilika ghafla na nyumba inawaka moto lakini haiteketei.”
“Kivipi sasa?”
Suma akaanza kumsimulia kila kitu. Hakuna alichomficha kuhusu kilichokuwa kikiendelea nyumbani kwake. Ustaadhi Alii alishajua kilichotokea. Akamuamrisha asimamishe gari haraka.
“Kwa nini?”
“Lazima niwapitie wenzangu kwanza.”
“Wako wapi?”
“Si mbali, ni hapo Tangibovu.”
“Kwa hiyo?”
“Twende, we fuata maelekezo yangu tu.”
“Sawa.”
Suma akaendesha gari kwa kasi ileile. Ustaadhi Alii akawasiliana na wenzake watatu. Ni walewale anaoshirikiana nao mara nyingi kwa ajili ya kufanya dua kunapotokea matatizo hasa yanayohusisha majini.
Kwa bahati nzuri katika mazungumzo yao walikubaliana wamsubiri barabarani kabisa kwa hiyo haikuwa shida sana kuwaona.
“Egesha pale, wale pale…” akasema Ustaadhi Alii.
“Sawa.”
Gari lilipofunga breki tu, tayari wale watu walishafungua milango na kuingia ndani ya gari. Tayari walishaelezwa dharura iliyotokea nyumbani kwa hiyo walifanya haraka haraka bila kupoteza muda.
Hapakuwa na mazungumzo ndani ya gari, Suma alikimbiza kama limeibiwa, robo saa tu baadaye alikuwa anaegesha nje ya geti lake. Aliogopa hata kuingiza ndani ya geti kwa kuhofia moto.
Walishuka wote watano; Suma, Ustaadhi Alii na wenzake watatu.
“Fungua mlango Suma,” Ustaadhi Alii akamwambia.
“Naogopa.”
“Huna haja ya kuogopa, fungua tu.”
Suma akasukuma mlango mdogo wa geti. Wakaingia kwa pamoja. Suma alikuwa akitembea taratibu huku akiogopa sana. Mazingira yalimshangaza sana. Nyumba ilikuwa kimya kabisa kama vile hapakuwa na kitu kilichokuwa kikitokea ndani.
Kwa moto aliouacha alitegemea kukuta tayari moto umeshasambaa nyumba nzima. Haikuwa hivyo. Kwa mwendo wa taratibu, Suma akatembea hadi barazani kwake na kusimama hapo kisha akamwangalia Ustaadhi Alii akionekana dhahiri alitaka kusikia maelekezo kutoka kwake.
“Simama.”
Suma akasimama. Ustaadhi Alii akawaonyesha wenzake ishara akimaanisha kwamba wazungushe duara dogo kwa kushikana mikono. Wakafanya hivyo. Mara wakaanza kusoma dua kila mmoja kwa wakati wake. Zoezi hilo liliendelea kwa dakika tano kisha baadaye wakaanza kusoma kwa kuelekezana…
Suma alibaki amesimama palepale barazani akiwa ameiinua mikono yake juu akimuomba Mungu akubali dua ile ili mabalaa yamuondoke. Alikuwa kwenye wakati mgumu sana.
Baada ya muda, dua ikamalizika. Suma akawakazia macho kusikiliza maelekezo mengine.
“Iingia ndani Suma,” Ustaadhi Alii akamwambia.
“Naogopa moto.”
“Hakuna moto.”
Suma akafungua mlango na kuingia sebule, wale watu wakiongozwa na Ustaadhi Alii nao wakaingia. Wote kwa pamoja wakaketi kwenye viti vilivyokuwa pale sebuleni.
“Vipi, moto uko wapi sasa?”
“Ulikuwa unatokea chumbani.”
“Haya fungua huo mlango wa chumbani.”
“Hapana hapana, hilo siwezi kufanya.”
“Suma.”
“Naam Ustaadhi.”
“Fungua mlango wa chumbani.”
Suma kwa woga sana akausogelea na kuufungua ule mlango, akaangalia ndani…hapakuwa na moto na kila kitu kilikuwa vilevile. Alijikuta akipiga kelele kwa hofu. Ustaadhi Alii akamfuata nyuma na kuingia kule chumbani.
“Usiogope tumeshasoma dua, hakuna madhara yoyote humu ndani,” akasema Ustaadhi Alii.
“Hata mimi nimeamini.”
“Hebu sasa turudi sebuleni.”
“Sawa.”
Wakaongozana hadi sebuleni, wakaketi kwenye viti. Utulivu wa muda ukapita wote wakiwa hawazungumzi chochote. Ustaadhi Alii alionekana kuwa na mawazo sana, alikuwa kwenye fikra nyingi sana akijaribu kuwaza juu ya tukio lile.
“Ni kweli umedhamiria kubadilisha mfumo wa maisha yako?” Ustaadhi Alii akamwuliza Suma.
“Ndiyo Ustaadhi.”
Akatulia tena kwa muda. Alimeza funda kubwa la mate, kisha midomo yake ikaanza kutingishika. Ni dhahiri sasa alidhamiria kuanza kuzungumza tena. Kweli, Ustaadhi Alii alikuwa akizungumza…
“Si umesema mkeo ndiye aliyekuwa akikutokea na kupiga makelele kuwa umemtesa na kumsababishia maumivu?”
“Ndiyo.”
“Una uhakika ni yeye?”
“Kabisa.”
“Kuna kitu nahisi, lakini kabla sijafika huko nataka kuuliza jambo moja la msingi sana.”
“Ndiyo niulize tu.”
“Huyo mkeo ulimchunguza vizuri kabla ya kuoana?”
“Sana Ustaadhi, sana.”
“Ulifunga naye ndoa?”
“Tena nyumbani kwao, mbele ya wazazi wake.”
“Sawa, hebu turudi katika upande wa pili…mambo yote haya yanayotokea yana sababu zake bila shaka. Unaweza kutusimulia vizuri ili tuweze kupata mwanga zaidi wa kumaliza tatizo lako?”
“Bila shaka yoyote Ustaadhi.”
“Enhee…unaweza kuanza basi, sisi tunakusikiliza,” akasema Ustaadhi Alii.
Wote walikuwa kimya wakijiandaa kumsikiliza Suma. Ni kweli alionekana kuwa na kitu kikubwa sana katika maisha yake. Suma alidhamiria kueleza ukweli wa ndani kabisa. Hakuwa na haja ya kuficha kitu chochote.
“Ni kweli ni stori ambayo huwa sipendi kabisa kuikumbuka, lakini kwa sababu nimeshaamua kubadilika na kuanza maisha mapya, inanipasa sasa nieleze kilichotokea…” akasema Suma.
“Sawa.”
“Lakini naamini kuna sehemu zinaweza kuwachukiza, naomba unisamehe maana nitawaeleza ukweli wa kila kitu kilichopata kutokea katika maisha yangu ya nyuma.”
“Usiwe na wasiwasi juu ya hilo Suma.”
Suma aliangalia juu, kisha akarudisha macho yake tena chini akitafakari mahali pa kuanza kueleza historia yake. Alifikiria kwa muda, hatimaye alipata mahali pa kuanzia.
“Nakumbuka vizuri sana…ilikuwa ni Moshi…” Suma akaanza kusimulia.
***
MOSHI – KILIMNJARO
Suma aliendelea kukaza macho kwenye ubao wa matangazo ya sinema nje ya kibanda cha kuonyesha muvi cha Baba Lau Cinema. Aliendelea kukaza macho yake kwa umakini mkubwa kama vile alikuwa akitafuta kitu muhimu.
Ni kama mwanafunzi aliyekuwa akiangalia majina ya watu waliochaguliwa kujiunga na chuo fulani wanavyofanya. Haikuwa hivyo, alikuwa akiangalia ratiba ya filamu zitakazoonyeshwa hapo kwa Baba Lau.
“Mh!” akaguna Suma baada ya kuangalia sinema itakayooneshwa saa 8:00 mchana.
Ilikuwa ni sinema ya Jack Chun. Akashuka chini kukaza macho tena. Akaangalia kwa umakini zaidi…
Saa 10:00 – Delta Force
Saa 1:00 Anold Schwarzenegger
Saa 3:00 Amitha Batchan
“Aaaah! Huyu jamaa bwana sijui vipi?” akasema kwa sauti kubwa kiasi kisha akasonya kwa hasira.
Suma hakuzipenda kabisa hizo sinema. Ilikuwa tofauti sana na wenzake waliokuwepo pale, walionekana kufurahishwa sana na ratiba hiyo.
“Daaah! Siwezi kukosa kumwangalia Amitha, lazima nije…” mmoja wa vijana waliokuwa pale akasema huku akimwangalia mwenzake.
“Tatizo ni ndefu sana, kwanza angalia muda wenyewe,inaanza saa tatu usiku, kuisha kwake ni hadi saa sita!”
“Hata kama ni mpaka asubuhi, mimi lazima nije. Huyu jamaa ananikosha sana. Kwanza sinema zao hazichoshi…kidogo wanapiga na wimbo kabisa. Yaani safi sana!”
“Kuchukuchu hotahe….ha ha ha ha…acha kunichekesha wewe!”
“Nyie mnazungumza nini?” Suma akapaza sauti.
“Kwani vipi Suma?”
“Mimi sijaona sinema ya maana hata moja hapo.”
“Unataka filamu gani sasa?”
“Mambo yangu huyajui?”
“Nini?”
“Vampire!” (Majini)
“Aaaah! Mimi naogopa sana kuangalia filamu za majini.”
“Sasa mimi ndiyo huniambii kitu kuhusu hizo filamu, yaani hapa sina raha kabisa, ngoja niondoke zangu,” akasema Suma huku akianza kupiga hatua za taratibu kuondoka mahali pale.
Kabla hajageuka, Baba Lawrance ambaye alifupishiwa jina na kuitwa Baba Lau alitokea…
“Afadhali nimekuona Baba Lau.”
“Suma hata salamu?”
“Nilijua ningekusalimia tu….shikamoo mzee.”
“Marhaba, vipi kuna tatizo?”
“Tena kubwa sana.”
Baba Lau akashtuka sana. Alitumia dakika nzima kutafakari hilo tatizo kubwa. Mawazoni mwake aliamini Suma alikuwa ameibiwa ndani ya banda lake la video. Akamkazia macho sawasawa.
Sauti yake ilikuwa kavu iliyotoka kikakamavu wakati akimwuliza Suma kwa mara ya pili…
“Lipi hilo?”
“Kwa nini hamna usawa?”
“Kivipi?”
“Mimi ni mteja wenu wa siku nyingi sana, lakini mbona mnaweka filamu za aina moja tu?”
“Kwani wewe unataka filamu gani?” akauliza Baba Lau ingawa alishajua kuwa alihitaji nini.
“Nataka sinema za majini, unajua zile zinafundisha mambo mengi ndiyo maana napenda kuangalia, halafu sipo mwenyewe, wengi tu wanapenda filamu za hivyo.”
“Sawa nimekuelewa vizuri Suma, kesho nitaweka.”
“Haya ahsante sana,” akasema Suma huku akiaga.
***
Ilikuwa ghafla tu, hata leo hii ukimwuliza Suma ni kwa nini anapenda kufahamu kuhusu majini, hajui. Kuna tukio moja ambalo halikumbuki. Ni siku aliyoangalia filamu ya majini yenye hadithi ya mapenzi iitwayo Even Devils Loves (Hata Majini Wanapenda).
Ni filamu hiyo ndiyo iliyobadilisha mtazamo wake kuhusu mapenzi. Ilikuwa na hadithi inayoonesha namna ambavyo majini wanaweza kupenda, kujali na kumthamini mwanadamu bila kumdhuru.
Mapenzi ya majini katika sinema hiyo, yalikwenda mbali zaidi na kuonesha namna ambavyo yanaweza kubadilisha maisha ya mtu ambaye ameingia naye kwenye mapenzi. Akajikuta akitamani kuwa yeye!
Msisimko alioupata ulikuwa mkubwa sana.
Pamoja na kufikisha umri wa miaka 22, akiwa tayari ameshamaliza elimu yake ya kidato cha nne, hakufikiria kabisa suala la kuoa binadamu. Alitamani kuoa jini.
Aliamini hao ndiyo wangeweza kuwa na upendo wa dhati, wasingemtesa wala kumnyanyasa. Hapo ndipo kulipokuwa na tatizo.
Kwa Mkoa wa Kilimanjaro, tena akiwa anaishi katika Manispaa ya Moshi Mjini, katika kitongoji maarufu cha Njoro, stori za majini hazikuchukua nafasi kubwa sana kwa wakazi wa eneo hilo.
Alikulia mikononi mwa wazazi wake wenye kipato cha kawaida kabisa, tena wakiwa wanaishi nyumba ya kupanga hapo Njoro. Walichoweza kufanya kwake, ilikuwa ni kumsomesha kwa uwezo wao wote. Kwa fedha za kuokoteza kwa kufanya biashara ndogondogo na vijibarua visivyo na uhakika!
Alisoma Shule ya Msingi Njoro na baadaye akachaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari JK Nyerere ambapo kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuchaguliwa na elimu ya juu zaidi kwa sababu alipata dalaja la nne!
Kwa namna alivyofundishwa na wazazi wake, kwa Suma maisha hayakuwa magumu sana, kwani aliamua kufanya vibarua mbalimbali ili aweze kujikimu. Hakutaka kujihusisha kabisa na mambo ya wasichana.
Alikuwa na msimamo mkali sana kuhusu mambo ya wasichana. Jambo hilo liliwashangaza wengi wakiwemo wazazi wake, maana hata siku moja, hawakuwahi kusikia Suma alikutwa amesimama na msichana mahali.
Miaka mitatu ilipita baada ya kumaliza kidato cha nne, kwa kudunduliza fedha zake, aliweza kupanga chumba chake na kununua vitu vyake vya ndani kisha akahamia Kitongoji cha Majengo. Wengi waliamini Suma alihama kwa lengo la kukwepa maneno ya watu.
Hilo hakujali.
Aliangalia sana maisha yake na namna alivyotamani yawe. Siri kubwa ilikuwa ndani ya moyo wake. Ni kweli alitamani sana kuoa, lakini si binadamu. Alitaka jini! Angempataje? Hilo lilibaki kuwa swali gumu lililomtesa kichwa chake.
“Yes…even devils loves,” (Ndiyo…hata majini wanaweza kupenda) aliwaza Suma akikumbuka sehemu ya jina la ile sinema aliyoiangalia.
“Kwa nini nisioe jini? Mimi sitaki usumbufu na hawa binadamu wenzangu,” akawaza Suma.
“Halafu maisha magumu niliyonayo, nitawezaje kuogeza mtu mwingine wa kunitegemea ambaye naye atazaa wengine na kunizidishia machungu katika hii dunia yenye ubaguzi?
“Ona wenzangu…mbona wanaishi vizuri. Wana majumba ya kifahari, magari na biashara za uhakika…mimi nitawezaje? Nahitaji msaada hakika na mahali pekee nitakapoweza kupata ni kwa majini. Lazima nitampata tu,” akazidi kuwaza Suma.
Ni mawazo yaliyomtesa sana kichwa chake. Hakutaka mateso wala shida maishani mwake. Alihitaji kustarehe na kutulia. Alihitaji faraja ya moyo hakika. Kwake, hapakuwa na binadamu ambaye angekuwa na uvumilivu kama majini aliowaona kwenye sinema za majini.
“Lazima hilo litimie,” akazidi kuwaza.
***
Walikuwa wanawake wawili tu barabarani, wakitembea kwa miguu, vikapu vikiwa juu ya vichwa vyao. Walitokea kununua mahitaji katika soko maarufu la vyakula mjini Moshi – Mbuyuni. Walishavuka kwenye mto mdogo unaopitisha majitaka maarufu kwa jina la Maji Machafu, wakishika njia pembeni ya kiwanda cha zamani cha Pepsi.
Hawa ni mama Suma na mama Mwaija. Kama kawaida ya wanawake, walizungumza mengi sana. Waliongelea ndoa, wakajadili kuhusu maisha na baadaye wakaanza kuwateta watu. Stori zilipoisha, mama Mwaija akaanza mpya…
“Halafu mwenzangu kuna jambo nimelisikia mitaani limeniuma sana, nimelivumilia sana lakini naona limenifika hapa, siwezi kuacha kukuambia, wewe ni shoga yangu.”
“Nini hicho mama Mwaija?” akauliza mama Suma.
“Ni kuhusu mwanao.”
“Yupi sasa? Mwenyewe unajua nina watoto wanne.”
“Suma.”
“Nini tena?”
“Hivi mtoto wenu mzima kweli?”
“Kivipi yaani?”
“Maneno niliyoyasikia, mbona yanatisha? Inasekana eti hawezi kitu!”
Mshtuko mkubwa ukaingia moyoni mwa mama Suma. Zaidi ya mara tatu neno lile likajirudia kichwani mwake; ‘Hivi mtoto wenu mzima kweli?’. Maumivu yasiyoelezeka yakauvamia moyo wake. Hata hivyo hakujua uzima uliozungumziwa.
Alitaka kufungua kinywa chake aulize, akahisi kama kuna kitu kinamkaba na kumzuia kufanya hivyo.
“Mwanangu anaumwa nini?” akajiuliza mwenyewe.
“Lakini haina maana kuumiza kichwa wakati naweza kuuliza,” akajisemea moyoni.
Ukweli ni kwamba siyo hakuweza kuuliza ila aliogopa na hakuwa tayari kusikia tatizo la mwanaye mpendwa. Ya nini ajitese? Kwa nini abaki na maswali? Akaamua kuvunja ukimya…
“Kivipi yaani?”
“Maneno niliyoyasikia, mbona yanatisha? Inasekana eti hawezi kitu!” mama Mwaija akagongelea msumari.
“Mh!”
“Unaguna nini mwenzangu, ndiyo mambo yanayosemwa huko mitaani.”
“Unadhani ni kwa nini wanasema hivyo?”
“Haya mambo yameanzia mbali, inasemekana kwanza hajawahi kuonekana na mwanamke yeyote wa mtaani, halafu kingine ilifikia hatua Tatu akamwambia wazi kuwa anampenda, mwanao akamtukana sana nusu ampige kwa sababu eti alimwambia mambo ya kijinga!”
Mama Mwaija alikuwa anamzunguzia Tatu, mtoto wa mzee Mvungi ambaye anasifika kwa uzuri mtaa mzima. Watu wenye fedha zao waligongana vikumbo kumgombea msichana huyo bila mafanikio. Leo hii eti Suma anatamkiwa na malkia huyo kuwa anampenda halafu anamkataa!
Lazima ushangae!
“Mh! Lakini labda hajamtaka!” akajibu mama Suma kwa lengo la kujiondolea aibu.
“Sawa ila sasa hata akiwa na wenzake, wakianza kuzungumzia mambo ya wasichana huonekana anakasirika na kuondoka zake.”
“Sina uhakika na hili jambo.”
“Usinitaje, mimi nimekuambia tu kama shoga yangu. Sisi wote ni wazazi.”
“Sawa.”
“Lakini jambo lingine linalowashtua zaidi watu ni tabia yake ya kujipenda kupita kiasi. Muda wote msafi, ananukia marashi, ananyoa vizuri, anavaa nguo nzuri…kwanini ajipende hivyo kama mtoto wa kike? Mchunguze mwanao shoga yangu!”
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia keshokutwa IJUMAA.