The House of Favourite Newspapers

Rais Samia: Maafisa Wenye Vitambi Warudi Kupata Mafunzo Waondoe Vitambi

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

AKIENDELEA na ziara yake jijini Tanga, Rais Samia leo hii amefunga mafunzo ya awali ya Jeshi la Uhamiaji pamoja na kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi unaondelea kwenye chuo hicho kilichojengwa eneo la Boma KichakaMiba wilayani Mkinga mkoani humo.

 

Wanajeshi wa jeshi jipya la Uhamiaji zaidi ya 818 wamehitimu mafunzo hayo.

 

Wakati wa hafla hiyo Rais Samia amelipongeza jeshi hilo la uhamiaji kwa kufikia hatua ya kujenga chuo hicho pamoja na kila aliyehusika katika kufanikisha ujenzi wa chuo hicho ikiwemo serikali.

 

Pia Rais Samia amevihakikishia kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama ili viweze kutekeleza vyema kazi zao za ulinzi wa Taifa, pia ameahidi kutoa ajira kwa wahitimu wa mafunzo na kuongeza vyeo kwa kadiri uchumi utakavyoruhusu.

 

Kwa upande mwingine Rais Samia amewataka wahitimu hao kuyaishi kwa vitendo mafunzo waliyoyapata kwenye chuo hicho na kusema kuwa ameona mapungufu kwa watendaji waliopo makazini hivyo akapendekeza wale walio ofisini warudishwe kwenye chuo hicho wakapate mafunzo ili kupunguza vitendo vya rushwa na uzembe katika maeneo ya kazi.

 

Pia, Rais Samia amependekeza ushirikiano kwenye mafunzo kwa jeshi hilo na majeshi mengine pamoja na kubadilishana askari kati ya Zanzibar na Tanzania bara ili kuondoa kujuana na kuongeza ufanisi wa kazi.

Kamanda wa Uhamiaji akitoa heshima mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Akisisitiza umuhimu wa askari walioko makazini kurudi mafunzoni Rais Samia alisema:

“Nimeangalia gwaride, maafisa waliokuwa wakiongoza vikosi vile ni maafisa ambao ni wazoefu lakini kati yao nimeona wanavitambi, nadhani hatutakiwi kuwa na maafisa wenye vitambi. Warudi tena hapa waje watoe vitambi ili wawe wepesi zaidi katika kutekeleza majukumu yao”

 

Jukumu la Jeshi la Uhamiaji ni kuwezesha na kudhibiti utokaji na uingiaji nchini wa raia na wageni kufuatana na Sheria Na. 7 ya 1995, Sheria ya Uraia wa Tanzania Na. 6 ya 1995 na Sheria ya Pasi na Nyaraka za Kusafiria Na. 20 ya mwaka 2002 na Kanuni zinazoambatana na Sheria hizo.

 

Imeandikwa: Abdallah Kaputi kwa msaada wa mitandao.

 

Leave A Reply