Stanbic Yatoa Wito wa Uwekezaji Katika Sekta ya Nishati na Ushirikiano wa Kikanda
Kadiri Afrika Mashariki inavyoelekea katika zama mpya za mageuzi ya sekta ya nishati, Tanzania inachukua nafasi muhimu katika kuunda mustakabali wa sekta hii katika kanda hii imeelezwa jijini Arusha.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa tano wa Ushirikiano wa Nishati Afrika Mashariki (EA-ECS) 2025, jijini Arusha, Joe Mwakanjuki, Makamu wa Rais, Nishati na Miundombinu, Stanbic Bank Tanzania, alisisitiza umuhimu wa uwekezaji makini katika miundombinu ya nishati ili kuchochea maendeleo endelevu.
Alisema kwa upande wao Stanbic Bank Tanzania wakiwa wadhamini wakuu wa mkutano huo wanathibitisha dhamira yao ya kuwezesha uwekezaji, katika miundombinu muhimu, na kusaidia maendeleo ya viwanda kama vichocheo vya ukuaji wa uchumi.
Kaulimbiu ya EA-ECS 2025 ni “Kuwezesha Afrika Mashariki: Kufungua Uwezo wa Nishati wa Tanzania kwa Soko la Nishati la Kikanda,” mkutano huu wa siku mbili, huwakutanisha viongozi wa serikali, wawekezaji, na wataalamu wa sekta ya nishati ili kujadili suluhisho za kupanua upatikanaji wa nishati, kuunganisha vyanzo vya nishati endelevu, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Pamoja na hayo Bwana Mwakanjuki alisema Benki ya Stabic Tanzania inatambua umuhimu wa uwezeshaji wa kifedha katika kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya nishati, kwa kutumia utaalamu wa Standard Bank Group, Stanbic imekuwa na mchango mkubwa katika kubuni suluhisho za kifedha zinazopunguza uhatarishi katika uwekezaji, kuwezesha ushirikiano wa kimkakati, na kuharakisha maendeleo ya miradi mikubwa ya miundombinu.
“Benki yetu imechangia katika miradi mikubwa ya nishati ikiwa ni pamoja na utafiti wa uchumi mkuu wa gesi asilia (LNG) nchini Tanzania.
“Nje ya mipaka ya Tanzania, Standard Bank Group imesaidia uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kufadhili mradi wa nishati upepo wa Seriti Green nchini Afrika Kusini, kupanua suluhisho za nishati mbadala kupitia CrossBoundary Energy, na kufanikisha uwezeshaji wa mradi wa nishati upepo wa Lake Turkana Wind Power nchini Kenya, ambao ni shamba kubwa zaidi la nishati upepo barani Afrika.
“Kushiriki kwa Benki ya Stanbic katika EA-ECS 2025 kunadhihirisha dhamira yetu ya kusaidia ukuaji wa Tanzania kwa kushirikiana na taasisi za serikali, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo ili kutatua changamoto za sekta ya nishati, kufungua fursa za uwekezaji, na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama mchezaji muhimu katika soko la nishati la kikanda”, alisema Bwana Mwakanjuki.
Kadri EA-ECS 2025 unavyoendelea kuweka mwelekeo wa mustakabali wa sekta ya nishati Afrika Mashariki, Stanbic Bank inasalia kuwa mshirika mkuu katika kuhakikisha kuwa dira ya Tanzania ya kuwa kituo cha nishati kikanda inatimia. Kupitia ushirikiano wa kimkakati, ufadhili bunifu, na dhamira ya muda mrefu kwa maendeleo endelevu, benki inalenga kuharakisha mabadiliko ya sekta ya nishati na kusaidia ustawi wa kiuchumi katika ukanda mzima.


Comments are closed.