Wanafunzi Watatu Wafadhiliwa Shahada ya Uzamili na ALAF
Jumatano 17 Desemba 2025: ALAF Limited leo imetangaza ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watatu wanaofanya Programu ya Shahada ya Uzamili ya lugha ya kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI).
Akizungumza wakati akikabidhi hundi kwa wanufaika hao watatu, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF LTD, Hawa Bayumi alisema hatua hiyo ni muendelezo wa juhudi za kampuni hiyo kukuza Kiswahili katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kote.
“Kiswahili ni moja ya tunu kubwa tuliyorithi kutoka kwa Muasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni lugha ambayo inazidi kuenea na kupata umaarufu duniani na hatimaye kutambulika kuwa ndiyo lugha itakayoleta mshikamano wa bara la Afrika, hivyo tumeona hatuna budi kuunga mkono juhudi za serikali katika kuikuza lugha hii adhimu”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekuwa na jukumu kubwa na muhimu katika kuandaa na kutekeleza Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika , ambazo Kampuni ya ALAF LTD inadhamini pamoja na makampuni yake dada yaliyoko nchini Kenya na Uganda na ambayo inawaunganisha waandishi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
“Sisi kama moja wapo ya makampuni yaliyopata mafanikio makubwa na kutambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kama zana muhimu ya maendeleo ya kitamaduni,kijamii na kiuchumi , tumeona umuhimu wa kukuza fasihi ya kiswahili na ndiyo maana tutaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kuikuza lugha hii”, alisema.
Aliwataja wanufaika wa ufadhili huo wa ALAF kuwa ni pamoja na Frank John Kaswahili, Yasenta Emanuel Dagati, na Veromina Boazi Kerato ambapo jumla ya ufadhili huo ni Tsh 11, 700,000.
Alitoa wito kwa wanufaika kutumia ufadhili walioupata vyema kwa kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye masomo yao ili wawe na mchango mkubwa katika kuikuza lugha adhimu ya kiswahili kupitia elimu watakayoipata.
Kwa upande wake Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umeishukuru kampuni ya ALAF kwa ufadhili huo ambao umesema kuwa ni sehemu ya maombi mengi yaliyofanywa na wanafunzi wengi.
“Kwa kawaida huwa kuna maombi mengi kutoka kwa wanafunzi kuhusiana na ufadhili huu lakini ni wanafunzi watatu pekee ndio wanaohufaika; kwa hili tunawashukuru sana ila tunaomba mfikirie jinsi ya kuongeza idadi ya wanufaika ili lugha ya kiswahili iweze kukua zaidi”, alisema Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (Taaluma) Prof. Baraka Maiseli
ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania katika kutoa suluhisho mbalimbali za ujenzi ikiwemo kutengeneza bidhaa za uezekaji kwenye majengo iliyoanzishwa mwaka 1960 na tangu wakati huo imekuwa kinara katika kutengeneza bidhaa za uekezaji pamoja na bidhaa zingine za chuma ukanda wa Afrika Mashariki.
Mbali na bidhaa za uekezaji ALAF pia ni kinara katika kutengeza bidhaa zingine za kama vile koili za chuma na mabomba ya chuma kwa ajili ya matumizi mbalimbali jambo ambalo linaifanya kampuni hiyo kuwa kinara katika sekta ya ujenzi ukanda wa Afrika Mashariki.


