Waziri Mkuu: Wanawake Mnaweza na Wanawake Wahandisi Mnaweza Zaidi

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa amewatia shime Wahandisi wanawake kuwa wanaweza na mchango wao una thamani kubwa kwa maendeleo ya nchi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Julai 29, 2022 katika Kongamano la Wahandisi Wanawake, ambalo limekuwa na lengo la kuangalia mchango wa Wahandisi wanawake nchini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaasa pia Wahandisi hao kuendelea kuwa na utaratibu wa kufanya makongamano hayo kwani fursa kwa wanawake zinazidi kupanuliwa.

“Niendelee kuwatia shime kwa kusema kuwa wanawake mnaweza na wanawake Wahandisi mnaweza zaidi jipigieni makofi, nasema hili kwa sababu nimepata fursa ya kutembelea miradi kadhaa na miradi ambayo imesimamiwa na Wahandisi wanawake kwa uchache sana nilipata bahati ya kutembelea Daraja la Tanzanite Injinia aliyetoa maelezo kutoka mwanzo mpaka mwisho wa Daraja alikuwa mwanamke.” amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha Waziri Mkuu amesema anao ushahidi wa kuwa wanawake Wahandisi wanaweza zaidi na tayari Serikali ipo kwenye utekelezaji wa mikakati iliyoainishwa kwenye ilani ya chama cha Mapinduzi kwa kuhakikisha inaimarisha uwiano wa udahili wa wanafunzi wa chuo kikuu katika fani za uhandisi ili kuwapa nafasi kubwa wanafunzi wa kike kusoma fani za uhandisi.
Lakini pia Waziri Mkuu amebainisha kuwa Serikali imeelekeza kuhakikisha kuwa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa watoto wa kike iwe zaidi ya 35%.